WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo ufuatilie hatma za malipo ya kazi za wasanii na wampatie taarifa Katibu Mkuu wao.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Februari 8, 2020) wakati akizungumza na viongozi wa wizara mbili za Habari na Utamaduni, na ile ya Maliasili na Utalii na wa Chama cha Muziki wa Rhumba Tanzania (CHAMURUTA) kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake, Mlimwa, jijini Dodoma kuangalia namna muziki huo unavyoweza kutumika kutangaza utalii.
“Wakurugenzi nataka mfuatilie hatma ya malipo ya kazi zao. Hivi ni kwa nini mwimbaji wa Tanzania anatunga wimbo wake, unapigwa nchi nyingine Afrika au Ulaya, unauzwa kwenye CD ndani na nje ya nchi, wanafaidi wao lakini mwanamuziki wetu hapati malipo yoyote?”
“Nimewasikia wakisema Taifa fulani mwanamuziki anafaidika hata baada ya kufariki. Hivi Taifa hili wanafanya nini hadi wanafaidika na sisi tunafanya nini, hawa wanafaidika na sisi hatufaidiki. Ni kitu gani hicho kinawafanya wenzetu wananufaika na sisi wa kwetu wasinufaike?
“Msanii anapotoa kazi yake, labda ya muziki na unapigwa Kenya, kuna mfumo gani wa kuhakikisha nchi inapata mapato ili naye aweze kupata haki yake?” amehoji.
Waziri Mkuu amesema aliwahi kuwasikia akina Harmonise, Diamond na Ali Kiba wakisema kwamba wao wanaingiza kazi kwenye YouTube na wanalipwa, inakuwaje sasa wanamuziki wa rhumba wao nyimbo zao haziwekwi huko.
Amesema aliwahi kumsikia mke wa Mbaraka Mwinshehe akiomba Serikali imsadie apate haki kutokana na nyimbo za mume wake ambazo zinaigwa kila mara ili aweze kusomesha watoto. “Inakuwaje huyu mama anakosa hela wakati nyimbo za marehemu mumewe zinapendwa sana na zinapigwa kila mahali?”
“Wakurugenzi nenda mkafanye kazi yenu, leteni taarifa kwa Katibu Mkuu wenu na yeye ataifikisha kwa Waziri. Na kama itabidi kuileta Bungeni, tutalifanyia kazi ili wasanii wetu waweze kunufaika.”
Mapema, akijibu hoja ya kupatiwa mafunzo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Bi. Juliana Shonza alisema Wizara itaangalia ni aina gani ya kozi zinatolewa na Chuo Kikuu cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA) kwani ziko za muda mrefu na za muda mfupi.
“Tutamwambia Kaimu Mkurugenzi wa Sanaa ili awaandalie hayo mafunzo hasa ya muziki wa dansi. Tutahakikisha yanafanyika ndani ya mwaka huu na tutashirikiana nao kuhakikisha muziki wa rhumba haufi,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Costantine Kanyasu alisema wako tayari kushirikiana na wanamuziki wa rhumba kutangaza lakini akataka wafanye mabadiliko makubwa na wabadili mtazamo wao ili waweze kuendana na hali halisi ya soko la sasa.
“Bendi zetu zinahitaji kufanya mabadiliko makubwa ili kwenda na wakati wa sasa na kuweza kuwavuta watu wengi zaidi. Ni Lazima wanamuziki wafikirie muziki kiuchumi, waanze kwenda kidijitali zaidi kuliko kuwa jukwaani peke yake,” alisema.
Naye, Mlezi wa CHAMURUTA, Mzee Kikumbi Mwanzo Mpango (King Kiki) alisema kipaji alichonacho hajakipata kwa kusoma shule bali amepewa na Mungu, na ndiyo maana kiko kwenye damu.
“Niko tayari kuwafundisha vijana wengine kabla Mungu hajaniita, ili vipaji nilivyonavyo visipotee bure. Niko tayari kushirikiana na Serikali kuitangaza Tanzania, na kutangaza utalii,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CHAMURUTA, Dk. Salim Omar Mwinyi alishauri Serikali iangalie uwezekano wa kuanzisha maktaba ya kutunza ala za muziki ili kutunza kumbukumbu kwa vizazi vijavyo. Pia aliomba Serikali iwapatie mafunzo wanamuziki kwa kila mkoa ili waweze kuata uelewa wa mambo mbalimbali ikiwemo uongozi na utunzaji fedha.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU