WADHAMINI WAIOMBA MAHAKAMA ITOE KIBALI CHA KUMKAMATA TUNDU LISSU


Wadhamini wa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wamewasilisha maombi mahakamani kutaka itoa kibali cha Lissu kukamatwa baada ya kushindwa kumshawishi arejee nchini.


Akizungumza leo Alhamisi Februari 20, 2020 wakili wa Serikali mwandamizi,  Wankyo Saimon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa lakini  wameshapokea nyaraka iliyowasilishwa mahakamani.

“Shauri hili limekuja kwa ajili ya kutajwa limekuwa likikwama kutokana na mshtakiwa wa nne kutokuwepo na leo tumepokea maombi namba mbili ya mwaka 2020 yaliyowasilishwa na wadhamini wakiiomba mahakama itoe kibali cha kumkamata mshtakiwa,” amedai wakili Wankyo na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine ili maombi hayo kusikilizwa.


Robert Katula ambaye ni mdhamini wa Lissu aliieleza mahakama hiyo kuwa juhudi walizofanya ni pamoja na kuwasiliana na mshtakiwa bila mafanikio pamoja na kumuandikia barua mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwasaidia ili Lissu arejee nchini.


Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi March 2, 2020 kwa ajili yakusikiliza maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wadhamini na kuangalia sheria inasemaje.

Katika kesi ya msingi Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002..


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527