TANZANIA YASHINDA TUZO YA UTALII NCHINI INDIA

Tanzania imeshinda tuzo ya utalii kwa kuonekana ni eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori duniani nchini India kwa mwaka 2020 (The Best International Wildlife Destination).


Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka H. Luvanda amepokea Tuzo hiyo kutoka Jarida la kihindi la “Outlook Traveller Magazine” katika hafla maalum iliyofanyika katika Hoteli ya Roseate jijini New Delhi kwa niaba ya Tanzania. Hafla hiyo ilihudhuriwa na takriban washiriki 200. 

Tanzania imepata ushindi huo kutokana na kura zilizopigwa kwenye mtandao wa jarida hilo la “Outlook Traveller” lililoshirikisha wapiga kura 1,200,000 kwa njia ya mtandao.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushinda tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka nchini India, washiriki kupitia jarida hilo wameichagua Tanzania kama eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori duniani.

Aidha, Shelisheli na Indonesia kwa pamoja zilishinda tuzo kama maeneo bora zaidi duniani kwenye utalii wa fukwe.

The Outlook Traveller Award ni tuzo ya kifahari zaidi katika sekta ya utalii nchini India na hutolewa na Jarida la Utalii la “Outlook Traveller Magazine” ambalo ni jarida namba moja nchini India linalojishughulisha kutangaza utalii, ndani na nje ya India.

Wakati akipokea tuzo hiyo, pamoja na mambo mengine Balozi Luvanda aliushukuru uongozi wa Jarida hilo kwa kuandaa tuzo hizo muhimu ambazo zinasaidia kutanganza utalii wa nchi mbalimbali nchini India na akaeleza kuwa kupitia tuzo hiyo, watu wengi zaidi wataijua Tanzania na vivutio vingi vya utalii vilivyopo nchini na kuwavutia kutembelea Tanzania.

Mafanikio hayo yanatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini India, Wizara za Utalii za Tanzania Bara na Zanzibar, na Taasisi zote zinazosimamia masuala ya utalii za ndani na nje ya nchi katika kutangaza vivutio vya utalii kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo India.

Kupitia juhudi hizi, idadi ya watalii wanaokuja Tanzania kutoka India imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, idadi hiyo iliongezeka kutoka watalii 39,115 mwaka 2016 hadi watalii 69,876 mwaka 2017. 

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi zake ukiwemo Ubalozi wa Tanzania nchini India na wadau wengine itaendelea kuongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ili kuhakikisha idadi ya watalii kutoka India na nchi zingine duniani inaongezeka. Hii ni pamoja na kutumia Shirika la Ndege la Tanzania ambalo limeanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai kuanzia mwezi Julai 2019 kwa upande wa India.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post