SUGU AFUNGUKA BAADA YA MADIWANI WAKE 11 WA CHADEMA JIJINI MBEYA KUTIMKIA CCM


Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amemtumia salamu katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akibainisha kuwa madiwani 11 wa Chadema katika Jiji la Mbeya kuhamia chama tawala hakuwezi kubadili mapenzi ya wananchi wa Mbeya kwa Chadema.


Jumatatu, Dk. Bashiru akiwa jijini Dodoma, aliwapokea madiwani hao 11 kutoka Chadema walioongozwa na Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi, huku sababu kuu ya kutimkia kwao CCM ikidaiwa kuwa kuvutiwa na utendaji wa Rais John Magufuli.

Madiwani hao  na kata zao kwenye mabano ni Mwashilindi (Nzovwa), naibu Meya, Fanuel Kyanula (Sinde); Fabian Sanga (Ghana); Anyandwile Mwalwiba (Isanga);  Dickson Makilasa (Ilomba); Constantine Mwakyoma (Kalobe); Furaha Mwandalima (Ilomi); Anderson Ngao (Mwasanga); Ibrahim Mwampwani (Isyesye); Henry Mwangambaku (Forest) na Kigenda Kasebwa (Viti Maalumu).

Baada ya kuwapokea, Dk. Bashiru alisema mitambo aliyoweka ya majaribio kwenye mikoa jirani, imemfikia Mbunge wa Mbeya Mjini (Sugu), akifafanua zaidi kuwa:

Akizungumza jana kwenye mkutano wa viongozi waandamizi wa Chadema Kanda ya Nyasa uliofanyika jijini Mbeya jana, Sugu alidai kupigiwa simu na Dk. Bashiru baada ya madiwani hao kujiuzulu uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM.

Sugu alidai madiwani wote walioondoka Chadema, walikuwa wamekata tamaa ya maisha ya siasa.

“Juzi alinipigia simu Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, akitaka kujua hali yangu na nilichomjibu nilimwambia 'wewe ni rafiki na mtani wangu, lakini kwa sasa umekuwa ndugu kwa sababu umeniimarisha kisiasa kuliko wakati wowote,’ nilimwambia hivyo kwa sababu ametuondolea mizigo,” alisema.

Sugu alisema kuhama kwa madiwani hao 11 akiwamo Meya, Mwashilindi na Naibu Meya, Fanuel Kyanula, hakujakidhoofisha chama hicho, bali kumekiimarisha zaidi.

Alisema awali baada ya kupata taarifa ya madiwani hao kutimka, alipata wasiwasi kwamba chama hicho kitakuwa kimepoteza mwelekeo, lakini alipofanya utafiti mdogo kwenye baadhi ya maeneo, alibaini bado kinakubalika kwa wananchi.

Alisema hofu yake ilikuwa huenda madiwani hao walihama pamoja na wanachama, lakini utafiti wake ulibaini wameondoka peke yao na familia zao na sio wanachama wa Chadema ambao ndiyo wapigakura wake.

“Suala la ubunge na kura za urais Mbeya tulikwisha kulimaliza tangu mwaka 2010, wakiwa hawaamini basi wasubiri wataona,” Alisema.

Alidai Meya wa Jiji la Mbeya, Mch. Mwashilindi, alikuwa hashiriki kwenye shughuli za chama hicho kwa muda mrefu, akieleza kuwa hata mkutano mkuu wa Chadema uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana jijini Dar es Salaam hakuhudhuria.

Mbunge huyo alidai Chadema ina mtaji wa wapigakura zaidi ya 250,000 ndani ya jiji hilo, akibainisha kuwa 200,000 ni wanachama wa chama hicho na wengine zaidi ya 50,000 ni wanachama wa CCM na vyama vingine.

Alisema kupitia kampeni yao ya Chadema ni Msingi, chama hicho kimeandikisha wanachama zaidi ya 60,000 na kwamba mpaka kufikia Juni mwaka huu, kitakuwa kimeandikisha wengine 100,000 na mpaka kufikia tarehe ya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, kitakuwa na uhakika wa wanachama 200,000.

Kuhusu picha ambayo imekuwa ikizunguka mitandaoni ikimwonyesha yeye na baadhi ya vijana wa CCM, Sugu alisema ni ya mwaka 2017 wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambayo vijana hao walimwomba apige nao picha.

“Wale vijana baada ya kuniona mimi mbunge wao, waliniomba tupige picha, mimi nisingeweza kukataa kwa sababu najua wale ni wanachama wa CCM mashati, lakini mioyoni mwao ni wapigakura wangu japokuwa ile picha imeanza kutumika vibaya,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527