RAIS MAGUFULI: TUSIZUIE SHUGHULI ZA KIDINI NA BADALA YAKE YASHUGHULIKIWE MAPUNGUFU YALIYOJITOKEZA


Rais  Magufuli amesema shughuli za kidini ama kiimani, hazipaswi kufungwa kutokana na maafa ya vifo vya watu 20 mkoani Kilimanjaro, yaliyosababishwa na watu kukanyagana, wakiwahi kukanyaga mafuta ya upako, badala yake yashughulikiwe mapungufu yaliyojitokeza.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ametoa ujumbe huo wa Rais Magufuli jana wakati wa mazishi ya kitaifa ya watu 19, kati ya 20, yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa mjini Moshi. Watu hao walikufa baada ya kukanyagana walipokuwa wakifuata mafuta ya upako ya Mtume Boniface Mwamposa.

“Asubuhi wakati nazungumza na Rais kuhusu tukio hili, alisisitiza tushughulikie mapungufu yaliyojitokeza, badala ya kufunga shughuli za kiimani…mimi nasema tuzingatie vibali vyetu ili kuepusha maafa kama haya,” amesema Mghwira.

Alisema tayari Jeshi la Polisi, linafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo, ambapo pia viongozi waandamizi wa Mtume Mwamposa, wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Mghwira alisema pia baadhi ya watu, wanaodhaniwa ni vibaka, walikuwa miongoni mwa vyanzo vya watu kupata maafa hayo, kutokana na kitendo cha kujaribu kuwaibia waumini waliokuwa wakitoka mlangoni.

“Ninyi vibaka ambao ni sehemu ya maafa haya, lazima mjue damu ya watu iliyopotea na iliyomwagika, itakuwa juu yenu na malipo yenu yanakuja,” alisema mkuu wa mkoa.

Alisema tukio hilo limegusa pia wananchi wa mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Kwa upande wao, viongozi wa madhehebu ya dini, walisema wanapinga mfumo wa maombezi ya kidini, unaofanywa sasa kwa kasi, kwa kigezo cha kuleta uponyaji kwa waumini wao.

Aidha, viongozi hao waliomba serikali kutazama baadhi ya madhehebu, yanayotumia mgongo wa dini na ufahamu mdogo wa waumini katika kuwarubuni na kuwasababishia maafa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post