RADI YAUA MWANAFUNZI NJOMBE

Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wanafunzi 16 na mwalimu mmoja wa shule ya sekondari Chief Kidulile iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe wamepigwa radi februari 19 majira ya saa tisa alasiri na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na kuacha majeruhi 16.

Akifafanua kuhusu tukio hilo kwa njia ya simu,kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa akiwa mkoani Morogoro kikazi amesema amepokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa vijana wake aliowatuma ambapo  amesema katika tukio hilo mwanafunzi mmoja wa kiume amefariki dunia punde baada ya kukimbizwa hospitali na mwingine mmoja kujeruhiwa vibaya mguuni na jichoni huku pia akisema wengine 15 walipata majeraha madogo .

"Radi imepiga watu 17 mmoja wao amefariki kwa hiyo majeruhi ni 16 na hao 16 mmoja ni mwalimu,na huyo mtoto aliyefariki ana umri wa miaka 16 jinsia ni wa kiume,niwaombe tu watu wawe makini wakati wa hizi mvua"alisema Hamis Issa

Seil Morel ambaye ni mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Ludewa anasema madaktari walipokea watu 17 ambao ni wahanga wa tukio hilo ambapo katika jitihada za kunusuru uhai wao wamelazimika kutoa huduma usiku na mchana hatua ambayo imekuwa na matokeo chanya kwani wanafunzi 15 wameruhusiwa asubuhi akiwemo mwalimu huku pia akidai mmoja amefariki na mwingine mmoja akiendelea kupata matibabu zaidi kwa kuwa amejeruhiwa vibaya .

"Tulipokea majeruhi wakitokea shule ya sekondari Chief Kidulile,tulipata wanafunzi 17 wakiwepo wanafunzi wa kike 11 wanaume wawili na mwalimu mmoja wa kiume na pia kifo kimoja cha mwanafunzi wa kiume,ilipofika majira ya leo asubuhi tumeweza kuwaruhusu wanafunzi 15 mwalimu akiwepo lakini kuna mwanafunzi mmoja wa kike alipigwa shock ya miguu pamoja na jicho kwa hiyo bado yuko kwenye matibabu na ule mwili uko mochwari taratibu za mazishi zinaendelea"alisema Seil Morel

Nae mkuu wa shule ya sekondari Chief Kidulile Aloyce Kapelele anasema tukio hilo limeleta mshituko mkubwa shuleni hapo kwakuwa halijawahi kutokea na kwamba jitihada za kuweka vidhibiti radi zinafanyika huku kuhusu wanafunzi walioruhusiwa hospitali wanaendelea na masomo kama kawaida .


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post