MOI YALETA MITAMBO YA KISASA YA UPASUAJI UBONGO BILA KUFUNGUA FUVU

NA ANDREW CHALE

SERIKALI ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kwa dhati kuboresha Sekta ya Afya nchini na tayari imeleta mitambo ya kisasa ya Maabara ya upasuaji wa Ubongo bila kufungua fuvu (Angio Suite).

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Taasisi ya Mifupa (MOI), Patrick Mvungi ameeleza kuwa mitambo hiyo imewasili Nchini ikitokea Ujerumani ambapo ni juhudi za Serikali ya kuona wanasogeza huduma za kibingwa hapa nchini.

“Mitambo ya Maabara ya upasuaji wa Ubongo bila kufungua fuvu (Angio Suite) imewasili bandari ya Dar es salaam.

Mitambo, Vifaa vingine pamoja na ukarabati wa Chumba vimegharamiwa na Serikali kwa gharama ya Tsh Bilioni 7.9.” Alisema mkuu wa kitengo cha Uhusiano MOI, Patrick Mvungi.

Na kuongeza kuwa ujio wa mitambo hiyo ya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi na mataifa mengine hapa Barani Afrika wanaofika MOI kwa ajili ya matibabu.

“Taasisi ya Mifupa-MOI pia tunatoa huduma mbalimbali za kibingwa na kibobezi zikiwemo; Upasuaji wa Kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye Ubongo, Upasuaji wa Mgongo kwa kufungua eneo dogo.

Zipo pia huduma za Upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, Upasuaji wa kupandikiza nyonga bandia, Upasuaji wa kupandikiza goti bandia na Upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo alieleza Mkuu wa kitengo cha Uhusiano MOI, Patrick Mvungi.

Huduma hizo na nyingine katika taasisi hiyo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi na mataifa mengine barani Afrika ambapo awali walikuwa wakizifuata nje ya Nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527