Mkuchika Aitaka TIRA Kuhakikisha Kampuni Binafsi Za Bima Zinafanya Kazi Kwa Kuzingatia Sheria, Kanuni Na Taratibu Za Nchi

Na Happiness Shayo -Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst.) George H. Mkuchika ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuhakikisha kampuni binafsi za bima nchini zinajiendesha kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu ili kutoa huduma zenye ufanisi na ubora kwa wananchi.

Rai hiyo ameitoa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa Kamati ya Uongozi ya Mamlaka hiyo yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma leo.

“Kazi yenu ni kuhakikisha kampuni binafsi za bima zinalipa kodi na zinawalipa kwa wakati wananchi wanaopata ajali za moto, ajali ya gari na majanga mengineyo” Mhe. Mkuchika amesema.

Ameielekeza mamlaka hiyo kufanya ufuatiliaji katika baadhi ya kampuni binafsi zinazotumia muda mrefu kuwalipa wateja wanapopatwa na majanga.

“Serikali iliona umuhimu wa kuwa na chombo kinachodhibiti shughuli za bima nchini ili kuwasaidia wananchi wasiotendewa haki wanapofuatilia stahiki zao baada ya kukumbwa na majanga mbalimbali kwa hiyo nawaomba muwe wakali kuhakikisha wateja wa kampuni hizi wanapata haki zao kwa sababu ninyi ndio kimbilio lao wanapokuwa hawatendewi haki” Mhe. Mkuchika amesema.

Pia, Mhe. Mkuchika ameitaka mamlaka hiyo kusimamia vyema kampuni binafsi ambazo zina matatizo ya mtaji zijiondoe zenyewe ili kupunguza malalamiko ya wananchi wanaodhulumiwa haki zao wakati wa majanga.

Aidha, Mhe. Mkuchika amezikumbusha taasisi na mashirika ya umma nchini kuhakikisha yanatoa gawio kwa Serikali bila kusukumwa kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kutekeleza Utawala Bora.

Naye, Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Mussa Juma amesema kuwa mamlaka hiyo itaendelea

kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwezesha mchango wa sekta ya bima nchini ili kuongeza pato la taifa ikiwa ni sehemu ya kufuata misingi ya Utawala Bora.

“Mamlaka itatoa kinga ya bima kwa sekta zote za uchumi na wananchi dhidi ya majanga mbalimbali ya kiuchumi na kijamii” Dkt.Juma ameongeza.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imeandaa mafunzo ya maadili lengo ikiwa ni kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wa Mamlaka hiyo, kuongeza ufanisi na tija kwa taasisi hiyo katika kutekeleza sera ya Utawala Bora. Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wajumbe wa kamati ya uongozi na kamati ya uadilifu kutoka katika Mamlaka hiyo na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post