MAHAKAMA YASHINDWA TENA KUTOA HUKUMU YA MAXENCE MELO WA JAMII FORUMS

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa mara ya nne imeshindwa kutoa Hukumu juu ya kesi namba 456 inayomkabili Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa Jamii Forum Maxence Melo baada ya Hakimu anayeendesha shauri hilo kutokuwepo.

Hii Leo kesi hiyo ilitarajiwa kutolewa hukumu mbele ya Hakimu mkazi Mkuu, Thomas Simba. Melo anakabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo kosa la kushindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi na kuharibu uchunguzi kinyume na sheria.

Awali ilipangwa kutolewa Novemba 26, 2019 ikapangwa tena kutolewa Disemba 06, 2019; baadae ikapangwa kutolewa Jan 22, 2020 kisha ikapangwa kutolewa leo Feb 19, 2020. 

Wakili wa Serikali Faraji Nguka amedai leo Februari 19,mwaka 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi ,kuwa kesi hiyo ilipangwa kwaajili ya kutolewa hukumu lakini Hakimu husika hayupo kutokana na majukumu mengine. 


Wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai wako tayari kwa hukumu lakini kutokana na maelezo ya Wakili wa Serikali hawana pingamizi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 19 mwaka 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na hukumu itasomwa Aprili 2, mwaka huu. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527