JENERALI MABEYO AZINDUA MAKAO MAKUU YA JKT CHAMWINO DODOMA


Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama  Jenerali Venance Mabeyo amezindua Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma. 


Akizungumza leo Februari 26, 2020 wakati akizundua makao makuu hayo Jenerali Mabeyo amesema kuwa,  JKT imekuwa yakupigiwa mfano kwa utendaji  unaotokana na utekelezaji  mzuri wa miradi yote waliyokabidhiwa. 


“Nawapongeza JKT kwa kutekeleza kikamilifu miradi ya ujenzi wa ukuta wa Mirerani, Ujenzi wa ukuta wa Ikulu ya Chamwino, Ujenzi wa ukuta wa uwanja wa ndege Ngerengere,Ukamilishaji wa nyumba za Jeshi la Magereza Ukonga Jijini Dar es Salaam na miradi yote mliyokabidhiwa mlitekeleza kwa wakati, ubora na viwango hali iliyowajengea heshima “, Alisisitiza Jenerali  Mabeyo 


Akifafanua Jenerali Mabeyo amesema kuwa ni wakati muafaka kwa JKT kujipanga kwa kujiimarisha kwa kununua mitambo na vifaa zaidi ili kujenga uwezo wa kuendelea  kutekeleza miradi mikubwa pasipo kutegemea vifaa na nyenzo za kukodi au kuazima. 


Aliongeza kuwa ili kuendelea kujenga heshima ya JKT  kwa Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. John Pombe Magufuli  ni vyema utekelezaji wa miradi yote ukaendelea kuwa katika ubora unaotakiwa, uzingatiaji wa Sheria ya manunuzi na taratibu zote zilizowekwa na Serikali. 


Aidha, Jenerali Mabeyo amewaasa Maafisa na Watumishi wa Umma watakaotumia majengo ya makao makuu hayo kuyatunza ili yaweze kudumu kwa kuwa ujenzi wake umetumia rasilimali nyingi. 


Katika hatua nyingine Jenerali Mabeyo amesema kuwa JKT inapaswa kujipanga kwa kuwa itahusika katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Ulizi wa Taifa katika Wilaya hiyo. 


Uzinduzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT umefanyika Bwigiri Wilayani Chamwino mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Wakuu wa Jeshi hilo wastaafu, Maafisa wa ngazi mbalimbali,ss Watumishi wa Umma, Wananchi na viongozi wa Wilaya hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527