HUKUMU YA KESI YA UCHOCHEZI INAYOWAKABILI VIONGOZI CHADEMA KUTOLEWA MACHI 10, 2020


Mahakama Ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 10, mwaka huu kutoa hukumu ya kesi ya uchochezi dhudi ya viongozi nane wa Chadema akiwemo  Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho,Dk.Vicent Mashinji ambaye hivi karibuni  amehamia CCM. 


 Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba amesema sheria inaelekeza pande zote kufanya majumuisho ili kuisaidia mahakama kutoa uamuzi kwa kuangalia masuala ya kisheria yaliyoibuliwa wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo na wametoa maelekezo kwa pande hizo kuwasilisha hoja zao katika siku tano za kazi baada ya mahakama kukamilisha uchapaji wa nyaraka zilizopo kwenye kesi hiyo na kuwapatia.

Amesema, anatambua kesi hiyo inamvuto kwa jamii, hivyo ni lazima iishe ili kila mmoja aweze kuendelea na shughuli zake na kuongeza  "Majumuisho ya mwisho mnatakiwa muyawasilishe siku tano za kazi," amesema Hakimu Simba. 


Ameongeza kesi hiyo inakurasa zaidi ya 1,000 ambazo anatakiwa kuzipitia na kutoa hukumu hivyo hukumu ya kesi hiyo itatolewa Machi 10, mwaka huu saa 4:30 asubuhi. 


Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu,  Katibu Mkuu Chadema na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Jumla ya mashahidi nane wa upande wa mashtaka walifika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao ambapo mahakama iliwaona washitakiwa wote kuwa na kesi ya kujibu na walijitetea kwa kuleta mashahidi kumi na tatu. 

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527