CCM KAHAMA WAADHIMISHA MIAKA 43 KUANZISHWA KWAKE KWA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO


Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog 
Katika kuelekea katika maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imeanza kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano katika halmashauri za Ushetu,Msalala na Mji wa Kahama.


Akizungumzia ziara hiyo ya kutembelea miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Ushetu, jana Febuari Mosi,2020 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Kahama Thomasi Myonga amesema ziara hiyo imelenga kukagua miradi iliyoainishwa na kutekelezwa na serikali ya awamu ya tano ambayo ipo katika ilani ya CCM.

"Leo Febuari mosi tumeanza kukagua miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Ushetu ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya wilaya,ujenzi wa Makao makuu ya halmashauri,madarasa,visima na mabweni katika shule mbalimbali.

“Tumeamua kuadhimisha miaka 43 ya chama chetu kwa kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili kubaini namna ilivyotekelezwa na kama kunakasoro tuweze kuziainisha kwaajili ya kupatiwa ufumbuzi wa haraka”,alisema Myonga.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Kahama Emanuel Mbamange alisema watatembelea halmashauri zote mbili ili kukagua miradi yote ambayo imetekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli ambayo imedhamiria kutatua kero za wananchi wanyonge.

Alifafanua kuwa maadhimisho ya miaka 43 ya CCM yamebeba kauli mbiu isemayo tumeahidi,tumetekeleza na tunaahidi tena kuchapa kazi kwa juhudi,ubunifu na maarifa zaidi ambapo yanaenda sambamba na kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo zenye lengo la kusongeza huduma karibu kwa wananchi.

Awali akiikaribisha kamati ya siasa ya wilaya ya Kahama katika makao makuu ua Halmashauri hiyo nyamilangano, mwenyekiti wa Halmashauri ya ushetu Juma Ally Kimisha alisema kuwa halmashauri hiyo imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa asilimia 100 ambayo fedha zake zimeshatolewa na serikali kwa lengo la kuwasidia wananchi kupata huduma za kijamii,kwa mfano ujenzi wa zahanati vituo vya afya na miundombinu ya madarasa na barabara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post