ATCL YAANDAA SAFARI MAALUM KWA WAFANYABIASHARA


Na Mwandishi Wetu-MAELEZO.
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limeandaa safari kwa wafanyabiashara wazawa itakayofanyika Machi 4, 2020 kwenda Mumbai India kwaajili ya kukuza biashara baina ya nchi Tanzania na nchi hiyo. 

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa ATCL, Josephat Kagwirwa alisema kuwa safari hiyo itahusisha wafanyabiashara na abiria wa kawaida na lengo la safari hiyo maalum ni kukuza biashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuwaunganisha na soko la India.

“Katika mkakati wa Biashara wa ATCL ambao ulianza 2017 ambao utamalizika 2022, tumeandaa safari maalum kwa wafanyabiashara wazawa nchini kwenda India kwa jukwaa la kibiashara la siku mbili kuanzaia Machi 5 hadi machi 6,2020, fursa ambayo itawasaidia wafanyabiashara kupata fursa masoko kwani watatembelea maeneo mbalimbali ya biashara ikiwemo kituo maalum ambapo bidhaa zote duniani hufikia na kusambazwa”, alisema Kagirwa.

Kagirwa alisema kuwa tiketi zitapatikana kwa dola za kimarekani 500 ambayo itahusisha kusafiri kwenda Mumbai na kurudi Dar es Salaam pamoja na huduma za kutembelea masoko mbalimbali na dola 700 kwenda na kurudi, huduma za kutembelea masoko pamoja na malazi.

ATCL imekuwa mdau mkubwa wa wafanyabiashara katika masoko ya nje kwani mpaka sasa imefanya safari za kwenda nje takribani mara saba ambazo zimekuwa na tija kubwa.  

Serikali ya Awamu ya Tano hadi sasa imenunua ndege nane kwaajili ya kulifufua shirika la ndege la ATCL na matunda yake yanaanza kuonekana na miongoni mwake ni hili la wafanya biashara wa Tanzania kuanza kufaidi uwekezaji huo mkubwa.
 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post