WATOTO 404 WAFANYIWA UKATILI WA KINGONO IRINGA

Na Mwandishi Wetu Iringa

Mkoa wa Iringa kwa kipindi cha Januari mpaka Novemba 2019 umekuwa na matukio takribani 404 ya vitendo ya ukatili wa kingono kwa watoto ikiwa ni tatizo kubwa linalowakabili watoto katika malezi na makuzi yao nchini.

Hayo yamebainika mkoani Iringa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipotembelea vikundi vya malezi kwa watoto katika kijiji cha Kising’a kilichopo Wilaya ya iirnga mkoani Iringa.

Akitoa taarifa hiyo Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Saida Mgeni amesema kuwa mkoa wa Iringa unakabiliwa na matatizo mbalimbali na umekuwa ukiongoza katika masuala mabalimbali yasiyofaaa katika jamii ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Ameongeza kuwa Serikali ya mkoa wa Iringa imejipanga katika kuhakikisha inapambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto mkoani humo kwa kuhakikisha inaratibu utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya vitendo hivyo kwa wanawake na watoto.

Akizungumza katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Afya, Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali haijalala wala kufumbia macho suala la vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto bali inachukua hatua kali kwa wahusika wa vitendo hivyo wanaobainika.

Dkt. Ndugulile amezitaka Kamati za malezi ya mtoto mkoani Iringa na nchi nzima kuhakikisha wanatoa taarifa za vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kuhakikisha hawawafichi watuhumiwa na hawamalizani kifamilia kesi za ukatil wa kijinsia.

Ameongeza kuwa ni jambo la aibu kwa Tanzania ya viwanda kuwa na vitendo vya kikatili kutokea katika jamii zetu kwani ni kikwazo kikubwa katika kuhakikisha jamii inajiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

“Mkiona wanajamii miongoni mwenu wanataka kumalizana katika kesi za vitendo vya ukatili wa kijinsia toeni taarifa ili tukomehse vitendo hivi visiendelee nchini” alisema Dkt. Ndugulile

Dkt. Ndugulile amewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanakaa na kuzungumza na watoto wao na sio kuwapiga na kuwapa adhabu zinatazosababisha kupata ukatili wa kisaikilojia ambao ni hatari kwa malezi na makuzi yao na kuhakikisha watoto hao wanapata haki zao za msingi zilizopo kisheria.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527