WANAFUNZI 900 WA KIDATO CHA TANO NA SITA MKOANI TABORA WAPIGWA MSASA KUHUSU SEKTA YA ANGA NA TCAA

NA TIGANYA VINCENT

JUMLA ya wanafunzi 900 wa Kidato cha Tano na Sita mchepuo wa Sayansi katika shule za sekondari tatu za Mkoani Tabora wamepewa elimu juu ya kujiunga na sekta ya usafiri wa Anga pindi watakapoliza shahada zao za vyuo vikuu katika fani za Sayansi.

Mafunzo hayo ya siku moja yamehusisha wanafunzi 500 wa Shule ya Sekondari ya Milambo, 200 WA Tabora Wavulana  na 200  wa Tabora wasichana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Tabora mara baada ya mafunzo hayo, Afisa Habari wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini(TCAA)  Bestina Magutu alisema lengo la elimu hiyo ni kuwasaidia wanafunzi wanasoma masomo ya sayansi kuwa na uelewa mpana na kuchangamkia fursa ya masomo yanayohusu sekta ya anga.

Alisema lengo jingine ni kuwahamasisha ili waanze kujiandaa kwa ajili kusomea fani mbalimbali za sekta ya anga kama vile urubani , uongozaji ndege, ufundi wa ndege , usimamizi wa usalama wa usafiri wa anga na huduma kwa wateja.

Kwa upande wa Mkufunzi kutoka Chuo cha Usafiri wa Anga Thamarat Salim alisema sekta ya usafiri wa Anga hapa nchini inakuwa kwa kasi ni vema wanafunzi wanasoma masomo ya sayansi wakachangamkia fursa hiyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuelekea uchumi wa Kati.

Alisema kozi nyingi za sekta ya usafiri wa anga zinamtaka mwanafunzi anayetaka kusomea kozi hizo ni vema awe amesoma masomo ya sayansi.

Naye Mwalimu kutoka Shule ya Sekondari ya Milambo Euphrahim Daffa alisema mafunzo yanayotolewa na TCAA kwa wanafunzi wanachukua masomo ya sayansi yamesaidia kuwaelimu sio tu wanafunzi hata walimu ya kujua kuwa hata wanafunzi anayechukua Fizikia ,Kemia na  Bioloji ( PCB) anaweza kujiunga na kozi za sekta ya anga.

Alisema hatua imesaidia kuwafumbua macho na kutambua kuwa kusoma PCB sio tu atasomea masomo ya sekta ya afya na  kilimo au walimu pekee yake bali  hata sekta ya anga wanayofursa.

Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga  nchini Mkoa wa Tabora Daniel Nyimbo alitoa wito kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kuchangamkia fursa ya masomo hayo usafiri wa anga pindi zinapotangazwa katika vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini.

Alisema kumekuwepo na fursa za kupata ufadhili wa kusomeshwa na TCAA kupitia kufanya usahili na pindi wanaposhindwa kusomeshwa kwenye kozi mbalimbali na kusema kuwa wanapoona hivyo wameombe.

TCAA inaendelea na utoaji wa elimu ya sekta ya anga kwa ajili ya kuwahamasisha wanafunzi wengi kusoma masomo ya sayansi kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa Kati ambao msingi wake mkubwa ni viwanda.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527