GST YAIBUA MAENEO MAPYA UTALII WA JIOLOJIA.....KAMATI YATAKA SHERIA YA MRI KUHARAKISHWA


Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewezesha kuibuliwa maeneo Mapya ya Utalii wa Jiolojia kufuatia kukamilika kwa utafiti wa Jiolojia katika maeneo ya ramani  Nne (4) za Jiolojia  (QDS 38,39,52 na 53).


Hayo yameleezwa na Mtendaji Mkuu wa GST  Dkt. Mussa Budeba wakati akiwasilisha taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya upatikanaji wa fedha za maendeleo kwa taasisi hiyo kwa kipindi cha Nusu Mwaka  kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Dkt. Budeba ameeleza kuwa, GST ilifanya utafiti huo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na kuongeza kuwa, suala hilo limeongeza vituo vya utalii wa Jiolojia nchini.

Akizungumzia huduma za  maabara ya GST kwa wadau wa sekta ya madini, kilimo na ujenzi amesema kuwa, baada ya kufanya maboresho  mbalimbali ikiwemo ununuzi wa baadhi ya vifaa vya kisasa, kuboresha mifumo ya uendeshaji wa maabara na kutoa mafunzo kwa watumishi, GST iliweza kupata ITHIBATIya kimataifa ya uchunguzi wa sampuli za dhahabu kwa njia ya tanuru kutoka shirika la SADCAS.

Aidha, akizungumzia mafanikio ya taasisi hiyo ameyataja kuwa ni pamoja na kushiriki katika mashindano ya kuchakata visawe vya mbali (Remote Sensing) yaliyofanyika nchini Botswana na kushinda nafasi ya Nne ambapo mwakilishi mmoja kutoka GST alitunukiwa Cheti cha kuwa mkufunzi kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Dkt. Budeba ameyataja mafanikio mengine ni kuweza kukusanya na kuhakiki jumla ya taarifa 109 kutoka kwenye kampuni mbalimbali za utafiti na uchimbaji wa madini pamoja na kukamilisha kazi ya ugani wa jiolojia na jiokemia katika QDS 293 iliyopo katika maeneo ya wilaya ya Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi.

Akizungumzia tukio lililosadikiwa kuwa ni volcano lililotokea katika Kata ya Ndembezi Manispaa ya Mji wa Shinyanga, ameieleza kamati kuwa, uchunguzi uliofanywa na GST ulibaini kwamba kulikuwa na tope lililochanganyika na maji likiwa linabubujika kutoka ardhini na kutengeneza rundo kubwa la tope la udongo juu ya uso wa ardhi mfano wa kichuguu na kwamba tukio hilo kwa lugha ya kigeni hujulikana kama " liquefaction".

‘’Mheshimiwa Mwenyekiti matukio haya ni ya kawaida kutokea katika maeneo ambayo ni tambarare, yenye kiasi kingi cha maji ardhini na pindi pakitokea msukumo ama mgandamizo katika  matabaka ya miamba ardhini, husababisha chembechembe za udongo kuchanganyika na maji na kusababisha tope ambalo husukumwa kuja juu ya  uso wa ardhi ambapo tukio hilo hutokea,’’ amesema Dkt. Budeba.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula akizungumza katika kikao hicho, ameitaka kuharakishwa suala la kuandaliwa Sheria ya Chuo cha Madini kutokana na umuhimu wa chuo hicho kuzalisha wataalam wa sekta ya madini na kutaka zifanyike jitihada mahusus kukamilishwa suala hilo. Mwenyekiti Kitandula ametoa msisitizo baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutaka suala hilo kukamilishwa haraka.

Pia, Mwenyekiti na wajumbe wa kamati hiyo wameishauri wizara kupitia chuo hicho kuangalia namna ya kuzalisha wataalam zaidi na ambao watakuwa na uwezo wa kujiajiri wenyewe bila kutegemea ajira ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kushiriki katika shughuli za madini hususan kwenye uchimbaji.

‘’ Najua hili si jambo la leo lakini ni vizuri kama wizara mkaanza kulitafakari,’’ amesema Mwenyekiti, Kitandula.

Awali, akitoa taarifa kwa Kamati, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Madini Emmanuel Kapira ameieleza kuwa, tayari Rasimu ya Sheria ya kuanzishwa kwa Chuo cha Madini imeandaliwa na kupelekwa katika Mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Pia, Kapira ameieleza kamati hiyo kuwa, katika kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata mafunzo yanayotolewa chuoni hapo, kimetengeneza mfumo wa kufundisha kwa lugha ya Kiswahili kwa waajiriwa na wachimbaji.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema ipo haja ya wadau wa madini kujifunza elimu ya biashara ya madini  kwa kuzingatia fursa zilizopo katika sekta hiyo na kuongeza kuwa, suala  hilo linatoa nafasi nzuri  ya kibiashara na uwekezaji kupitia sekta ya madini . Aidha, Naibu Waziri Nyongo ameishukuru kamati hiyo kwa kuendelea kuishauri wizara ili iweze kusimamia vema sekta ya madini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akitolea ufafanuzi suala la maabara ya GST baada ya kupata ITHIBATI ya Kimataifa, amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kusaidia kutoa elimu kwa wadau  wa madini katika maeneo yao ili waweze kutumia maabara hiyo ikizingatiwa kuwa  gharama zake ni nafuu na ina viwango vya kimataifa.

Akizungumzia suala la Chuo cha Madini kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam, amesema pamoja na mambo mengine ni kukiwezesha kuwa bora zaidi na kuendesha programu zinazoendana na soko la ajira.

 Vikao kati ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Wizara ya Madini vilivyoanza Januari 20, vimehitimishwa leo Januari 22, 2020.

Chanzo: Wizara ya Madini



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527