NAIBU WAZIRI BASHE; HAKIKISHENI KILA MKULIMA ANAKUWA NA AKAUNTI BENKI

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akisisitiza jambo wakati wa kufunga Warsha ya kuwajengea uwezo Wenyeviti na Mameneja wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Miradi ya Pamoja iliyofanyika Jijini Dodoma, kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani, (kushoto) Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume Dkt. Benson Ndiege akifuatiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Bi.Theresia Chitumbi akieleza masuala ya Vyama vya Ushirika wakati wa Warsha ya kuwajengea uwezo Wenyeviti na Mameneja wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Miradi ya Pamoja iliyofanyika Jijini Dodoma hivi karibuni
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea na wajumbe wa Warsha ya kuwajengea uwezo Wenyeviti na Mameneja wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Miradi ya Pamoja iliyofanyika Jijini Dodoma, hivi karibuni
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani akielezea Sekta ya Ushirika nchini wakati wa Warsha ya kuwajengea uwezo Wenyeviti na Mameneja wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Miradi ya Pamoja iliyofanyika Jijini Dodoma hivi karibuni
Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe amewataka viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Miradi ya Pamoja kuhakikisha kuwa wakulima watakaouza mazao yao kupitia Vyama vya Ushirika wanakuwa na Akaunti za Benki kwa lengo la kuwawezesha kupata fedha zao kwa wakati na uhakika.

Mheshimiwa Bashe ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Januari 24, 2020 Jijini Dodoma alipokuwa akifunga Warsha ya kuwajengea uwezo Wenyeviti na Mameneja wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Miradi ya Pamoja iliyofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 22 Januari 2020 ambayo iliandaliwa kwa pamoja kati ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

“Hakikisheni kila mkulima anafungua Akaunti Benki ili iweze kumsaidia kupata fedha zake kwa wakati na uhakika, nafahamu wakulima wamekuwa wakicheleweshewa malipo yao bila sababu za msingi; tunataka tatizo hili litatuliwe mara moja,” alisema Mhe. Bashe

Naibu Waziri amesema kuwa Benki ziko tayari kuwahudumia wakulima bila gharama yoyote watakapofungua akaunti kwenye Benki hizo na kupitishia malipo ya mazao yao wakati wa kuyauza kupitia Vyama vya Ushirika na kuondoa udanganyifu na wizi unaofanywa na watendaji wa Vyama wasio waadilifu.

“Wakulima wamekuwa wakinyanyasika sana kwani kuna udanganyifu mwingi na wizi unaofanywa kwa wakulima wakati wa msimu wa mauzo. Katika maeneo mengine utakuta fedha inaletwa kwenye AMCOS lakini malipo hayafanyiki na badala yake mkulima anaambiwa kuendelea kusubiri kwa muda usiojulikana,” alisema Mhe. Bashe.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Bashe amevitaka Vyama vya Ushirika kuagiza Pembejeo kwaajili ya wakulima ili kurahisisha upatikanaji wake na kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima.

“Katika kuagiza Pembejeo ikiwezekana tumieni fedha zenu wenyewe badala ya kukopa Benki ambazo zinawatoza riba kubwa na mlipaji wa mikopo hiyo ni mkulima na hivyo kuendelea kumdidimiza badala ya kumkomboa,” alisema Naibu Waziri.

Aidha, Mhe. Bashe amewataka watu wote wakiwemo baadhi ya viongozi waliochukua mali za wanaushirika popote nchini wazirejeshe mali hizo kwenye Vyama vya Ushirika na kushindwa kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Lazima viongozi wa Ushirika tubadilike ili vyama vya Ushirika viweze kuchangia na kulifanya Taifa letu kufikia Uchumi wa Kati. Tunatakiwa kuwa na viongozi sahihi ambao ndio madereva, makondakta na wapiga debe sahihi kwenye Vyama vyetu,” alisema Mhe. Bashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527