MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) YATOA TAHADHARI YA MVUA KUBWA


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha kwa mvua kubwa katika mikoa mbalimbali nchini 


Taarifa ya TMA imesema mvua hizo kubwa zinatarajia kunyesha leo Jumamosi Januari 25, 2020 kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

“Angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa Mbeya, Njombe, Iringa, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Tanga, Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba,” imeeleza taarifa hiyo ya TMA

Imesema athari zinazoweza kujitokeza ni uharibifu wa miundombinu na mali kwa baadhi ya maeneo, baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, hatari kwa maisha ya watu kutokana na maji yanayotiririka kwa kasi au maji yenye kina kirefu, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kesho Jumapili Januari 26, 2020 TMA imesema mvua kubwa zitanyesha kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Jumatatu Januari 27, 2020 angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kigoma, Geita, Mwanza na Kagera huku Jumanne ijayo TMA ikitoa tahadhari ya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya Geita, Mwanza na Kagera.
Advertisement

Jumatano ya Januari 28, 2020 angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara, Simiyu, Mwanza na Shinyanga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527