NAIBU WAZIRI BASHE ATAKA WAKULIMA WA MAHINDI WASIINGILIWE KWENYE UUZAJI WA MAZAO YAO

Na Amiri Kilagalila-Njombe
Serikali imeendelea kuwapa uhuru wakulima wa zao la mahindi nchini kwa kuuza mazao yao sehemu yoyote na kwa bei yoyote bila kuwekewa vikwazo kama ilivyo kwa mazao mengine ya chakula na biashara.

Naibu waziri wa kilimo Hussein Bashe akiwa mkoani Njombe wakati akizungumza na wakulima wa matunda ya parachichi na mahindi katika ukumbi wa Turbo mjini Njombe,amesema hakuna kiongozi wa serikali atakayempangia mkulima katika uuzaji wa mazao.

“Kama naibu waziri wa kilimo debe la mahindi hata muuze elfu hamsini hakuna mtu atakayewaingilia katika kuuza mazao yenu.lazima tuiheshimu sekta ya kilimo kama sekta zingine zozote”alisema Waziri Bashe

Aidha waziri Bashe amewataka wananchi watakaoshindwa kutumia unga wa mahindi kwa sababu ya ghalama wawe huru kununua zao jingine la chakula kama mchele au mihogo kuliko kumnyanyasa mkulima wa Mahindi,na kuingilia sekta ya kilimo huku akiwataka wakulima kuongeza uzalishaji.

Katika hatua nyingine ameagiza kuundwa ushirika wa wakulima wa parachichi mkoani Njombe kutoka mtandao wa wakulima wa parachichi ili waweze kukopesheka na kutanua kilimo hicho kutokana na uwingi wa wananchi walioweza kuhamasika .

“Nimefurahi sana kuona huu umati unaolima parachichi,tunataka huu mtandao ugeuke kuwa chama cha ushirika cha wakulima wa parachichi na TADB ili mkopesheke lazima muwe kwenye ushirika,na mkiwa kwenye ushirika tutatengeneza mradi wa kutengeneza soko la uhakika na kujenga miundombinu ya kuhifadhi mazao ili mnunuzi anapokuja kununua asinunue mazo yaliyoharibika”alisema Bashe

Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amesema amekwisha weka utaratibu wa kuwashirikisha wakulima wa parachichi na na wanunuzi wa zao hilo ili kuweka utariatibu wa uuzaji wa parachichi utakaomuhakikishia mkulima  bei ya uhakika pamoja na kuwa tayari kushughulikia swala la uundaji wa ushirika.

Erasto Ngole ni mmoja wa wakulima wa parachichi mkoani Njombe amesema licha ya mkulima wa zao hilo kunyonywa na wanunuzi lakini ametoa shukrani zake kwa serikali kuendelea kupambana na kuwajali wakulima hao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527