MBUNGE WA CCM AFARIKI DUNIA...RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

 Rais wa Tanzania, John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Job Ndugai kufuatia kifo cha mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Rashid Akbar kilichotokea leo Jumatano Januari 15, 2020 mkoani Lindi.

Taarifa iliyotolewa leo na mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa katika salamu hizo, Magufuli ameelezea kuhuzunishwa na kifo hicho.

“Spika naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia ya marehemu, wabunge, wananchi wa Newala vijijini na wote walioguswa na msiba huu, nawaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi” amesema Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Bunge la Tanzania inamnukuu Spika Job Ndugai akieleza kuhusu kifo cha mbunge huyo, kutoa pole kwa wafiwa.

Inaeleza kuwa mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa na ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya mbunge huyo.

“Natoa pole kwa wafiwa wote wakiwemo familia ya marehemu, wabunge, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,” amesema Ndugai.

Awali taarifa ya katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoani Mtwara, Seleman Sankwa ilieleza kifo cha mbunge huyo.

“CCM inathamini na kutambua mchango mkubwa wa marehemu enzi ya uhai wake akiwa mbunge katika kuwatumikia wananchi wa Newala vijijini,” amesema Sankwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post