MANGULA ATOA ONYO KWA WANAOPITA KWA WANANCHI KUTANGAZA NIA YA KUGOMBEA UONGOZI


Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania bara Philipo Mangula ametoa onyo na kuahidi kuanza kuwachukulia hatua kali za kimaadili kupitia kamati za ngazi tofauti za siasa ndani ya chama wanasiasa wote ambao wameanza kupita kwa wananchi na kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali jambo ambalo ni kinyume na kalenda ya chama.

Mangula ametoa katazo hilo katika kikao cha halmashauri kuu ya chama wilaya ya Wanging’ombe ambacho kimeketi kwa lengo la kupokea ripoti ya utekelezaji wa ilani ya Chama kwa mbunge na mkuu wa wilaya hiyo katika kipindi cha 2015 -2020 ambapo amesema kufanya hivyo kunakiuka misingi na maadili ya chama na kuathiri utendaji wa viongozi waliopo madarakani na kupiga marufuku kutoa zawadi ama msaada wa aina yeyote bila mawasiliano na mwakilishi.

Awali wakiwasilisha ripoti ya utekelezaji mbunge wa jimbo la Wanging’ombe mhandisi Gerson Lwenge na mkuu wa wilaya hiyo Comrade Ally Kassinge wamesema licha ya uchanga wa wilaya hiyo lakini katika kipindi cha miaka mitano wamefanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu,umeme,viwanda ,miundombinu na uchukuzi na kuahidi kuendelea kuchapa kazi.

Nao baadhi ya wajumbe akiwemo Juma Nambaila na Paulina Samatta  wanakiri kuridhishwa na utendaji wa viongozi hao huku wakiwataka mwaka huu kuelekeza nguvu katika kusogeza nishati ya umeme na utatuzi wa migogoro ambao umekithiri katika wilaya hiyo.

Katika kikao hicho nae katibu wa siasa na uenezi wa chama hicho mkoa wa Njombe  Erasto Ngole anatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura ambalo limeanza kufanyika tangu januari mosi na kuhitimishwa januari 7.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527