BITEKO AKAMATA KIWANDA BUBU CHA UCHENJUAJI DHAHABU SHINYANGA


Ndani ya kiwanda bubu kilichokamatwa na kufungiwa na waziri wa Madini Dotto Biteko.
Baadhi ya mifuko zaidi ya 25 ya cabon iliyokamatwa kabla ya kuchenjuliwa katika kiwanda hicho.
Maafisa madini wakifunga kiwanda bubu cha Uchenjuaji dhahabu katika kijiji cha Bunango wilayani Kahama.
Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumaza na mwenyekiti wa kitongoji cha Mnara wa voda Masoud Bakari kijiji cha Bunango katika kata ya Bugarama.

Na Salvatory Ntandu - Kahama
Licha ya serikali kuboresha sekta ya madini kwa wafanyabiashara wadogo wa madini wilayani Kahama mkoani Shinyanga imebainika kuwa wapo ambao wamekuwa wakifanya shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu ikiwemo kuanzisha viwanda bubu na kuikosesha serikali mapato.

Hayo yalibainishwa Januari Mosi mwaka 2020 Waziri wa Madini Dotto Biteko katika ziara yake ya siku mmoja ya kushitukiza katika kijiji cha Bunango katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga baada ya kubaini kiwanda bubu cha kuchenjua dhahabu kilichopo katikati ya makazi ya watu.

“Kiwanda hiki kipo hapa katika nyumba hii tangu mwezi julai mwaka 2019 huku kikiendelea kufanya kazi,serikali imepoteza mabapo mengi tutachukua hatua kali za kisheria kwa miliki wa mtambo huu na nyumba hii”,alisema Biteko.

Sambamba na hilo Biteko aliwataka viongozi wa vijiji na Mitaa wilayani humo kuhakikisha wanawafichua wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara haramu ya madini ambazo zinafanyika katika makazi ya watu ambao hawana vibali wanaoikosesha serikali mapato.

“Niwaagize viongozi wa mkoa wa Shinyanga kuthibiti vitendo vya biashara haramu ya madini ambavyo vinaendelea kushamiri katika maeneo mbalimbali kwani mpaka sasa tumeshakamata viwanda bubu viwili vya uchenjuaji wa dhahabu ili kutokomeza vitendo hivi", alisema Biteko.

Hata hivyo Biteko aliagiza kukamatwa na kuhojiwa kwa Ofisa mtendaji wa kijiji cha Bunango Kajanja Kajanja na Mke wa mwenye nyumba iliyobainika kuwa na mtambo wa kuchenjulia dhahabu aliyefahamika kwa jina mmoja la Shule kuhusiana na kuhusishwa na tukioa hilo.

Masoud Bakari Balozi wa kitongoji cha mnara wa voda alisema alishatoa taarifa kwa mamlaka za kisheria kuhusiana na uwepo wa kiwanda hicho katika eneo lake lakini hakuona hatua zozote zikichukuliwa kwa wahusika.

“Kiwanda hiki kipo katika nyumba hii tangu julai mwaka jana kuna vijana wageni wanne ambao walikuwa wakifanyashughuli ya kuchenjua dhahabu hapa viongozi wote wa eneo hili wanajua tumelalamika sana kuhusiana kumwagwa ovyo kwa maji yenye kemikali kwenye makazi yetu”,alisema Bakari.

Katika ziara hiyo mifuko zaidi ya 35 imekamatwa ikiwa na Cabon zinadhaniwa kuwa na madini ya dhahabu katika kiwanda hicho huku mashine hiyo yenye uwezo wa kubeba kilo 500 za Cabon ikiwa tayari imewekewa mzigo kwa ajili ya kuanza kazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527