KILICHOENDELEA MAHAKAMANI LEO KESI YA TUNDU LISSU


Mdhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Robert Katula ameiambia mahakama kuwa wakati anamdhamini mshtakiwa huyo hakujua kama atapigwa risasi.

Katula ametoa madai hayo leo Jumatatu Januari 20, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.

Amesema Desemba 19 mwaka jana, mahakama iliamuru Lissu afike leo mahakamani lakini amefanya juhudi za kuwasiliana naye akawafahamisha kwamba atawasiliana na wakili wa chama lakini hadi leo kimya.

Mdhamini huyo ameomba apewe muda zaidi wa kuhakikisha anamfikisha mshtakiwa huyo mahakamani.

“Mheshimiwa wakati natoa ahadi kwamba nitahakikisha anafika mahakamani sikujua kama atapigwa risasi, tumemuandikia Mwenyekiti Freeman Mbowe barua atusaidie kumfikisha mshtakiwa nchini,” amedai Katula.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hadi Februari 20 mwaka huu na kuamuru kwamba mshtakiwa ni lazima afike mahakamani tarehe hiyo kabla mahakama haijatoa amri nyingine zenye nguvu zaidi dhidi ya wadhamini.

Mdhamini wa mwingine wa Lissu ni Ibrahim Ahmed.

Kesi hiyo ilifunguliwa Juni 14 mwaka 2016 baada ya muda mshtakiwa wa nne, Lissu akapata matatizo yaliyomfanya ashindwe kufika mahakamani.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post