IRAN YASITISHA UTEKELEZAJI WA MAKUBALIANO WA NYUKLIA YA MWAKA 2015


Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo Jumatatu imetoa taarifa ikitangaza kuwa imechukua hatua ya tano na ya mwisho ya kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia maarufu kwa kifupi kama JCPOA.

Taarifa hiyo imesema kuwa, kuanzia sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakuwa na kizuizi chochote katika shughuli zake za nyuklia ikiwa ni pamoja na kurutubisha madini ya urani, asilimia ya urutubishaji wa madini hayo, kiwango kinachorutubishwa na katika masuala ya utafiti na uchunguzi.

Kwa msingi huo katika hatua hii ya tano, Iran imetupilia mbali kizuizi muhimu zaidi cha shughuli zake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambacho kinahusiana na idadi ya mashinepewa zinazoruhusiwa kufanya kazi.

Iran imesema katika taarifa hiyo kwamba, tokea sasa miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia itafanya kazi kwa mujibu wa mahitaji yake ya kiufundi. 

Imesisitiza kuwa, Iran itaendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kwamba iwapo vikwazo vyote vitaondolewa na Tehran ikafaidika na maslahi ya JCPOA,  iko tayari kutekeleza tena vipengee vya makubaliano hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post