FAO YASEMA TUSIPOWADHIBITI NZIGE WANAOIKABILIA ETHIOPIA, KENYA NA SOMALIA WATASAMBAA


Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO limeonya kwamba nzige walioivamia Ethiopia, Kenya na Somalia sasa ni wimbi kubwa kuwahi kushuhudiwa hivi karibuni na lisipodhibitiwa kuna uwezekano wa kusambaa katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.


Wimbi kubwa la nzige walionekana kutamalaki angani na kughubika mashamba pembe ya Afrika, kwa mujibu wa FAO tayari limeshasababisha uharibifu mkubwa kwa kusambaratisha maelfu ya ekari za mazao hali ambayo inaathiri uhakika wa chakula katika nchi hizo ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingine nyingi ikiwemo kutokuwa na uhakika wa chakula katika baadhi ya maeneo.

Rosanne Marchesich kiongozi wa timu ya dharura na mnepo ya FAO anasema mlipuko wa safari hii wa nzige ni mkubwa sana, “Tunachojua kuhusu uvamizi huu wa nzige wa jangwani ni kwamba ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudia Ethiopia na Somalia katika kipindi cha miaka 25 na ni mbaya zaidi kushudiwa Kenya kwa zaidi ya miaka 70."

Hata hivyo amesema kiwango cha nzige hao kinatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine lakini kwa sasa nchi zilizoathirika zaidi ni Ethiopia , Kenya na Somalia na nzige wameshasababisha athari kubwa , na hofu ni kwamba wanavyoendelea kuvamia sehemu zingine za nchi hizo athari hasa katika uhakika wa chakula zitakuwa kubwa zaidi, lakini pia katika kilimo, na maisha kwa wakulima na wafugaji.

FAO imetoa wito wa kuwa na kampeni ya pamoja kukabiliana na janga hilo la nzige ikihofia kwamba janga linaweza kusambaa kwa nchi zingine za Afrika Mashariki.

“Kuna hatari ya kusambaa, nchi muhimu zaidi zinazoangaliwa hivi sasa ni Uganda na Sudan Kusini. Uganda haijawahi kukabiliana na wimbi la nzige tangu miaka ya 60, hivyo kuna wasiwasi kuhusu uwezo wa wataalam mashinani kuweza kukabiliana na janga hilo bila msaada toka nje. Na katika nchi kama Sudan Kusini tayari kuna asilimia 47 ya watu wasio na uhakika wa chakula.”

Ameongeza kuwa mbali ya zahma zingine zinazowakabili mabadiliko ya tabianchi yamekuwa kichocheo kikubwa cha nzige kuzaliana.

Pamoja na kufuatilia janga hili kwa karibu FAO inatoa msaada wa hatua za kuwadhibiti nzige hao kwa njia ya anga na ardhini lakini pia mbinu za kuweza kuwasaidia wakulima na wafugaji kuendesha maisha yao.

Pia imeonya kwamba mazingira ya kuruhusu kuzaliana bado yapo na ongezeko la nzige linaweza kuendelea hadi Juni mwaka huu 2020.

Umoja wa Mataifa waingilia kati
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura OCHA imesema imetoa dola milioni 10 kutoka katika mfuko wake mkuu wa dharura CERF ili kuongeza nguvu katika kupambana na mlipuko wa nzige wa Jangwani ambao wamevamia maeneo kadhaa ya Afrika Mashariki. 

Akizungumza  na vyombo vya habari mjini Geneva Uswisi, Msemaji wa OCHA Jens Laerk amesema,“Ni mlipuko ambao uko Afrika Mashariki na pembe ya Afrika. Pia umebainika kusini magharibi mwa Asia na Bahari ya shamu, ni mlipuko mbaya wa aina yake katika miaka 25 kwa Ethiopia na Somalia na ni mbaya zaidi kwa Kenya kuwahi kuuona katika miaka 70. Madhara katika nchi hizo ni mabaya kwa kuwa malisho na mazao yanatoweka katika jamii ambazo tayari zilikuwa zinakabiliwa na upungufu wa chakula.”

Credit: Umoja wa Mataifa


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post