BUNGE LA MAREKANI LAJARIBU KUMZUIA TRUMP KUISHAMBULIA IRAN


Baraza la Wawakilishi la Marekani linalodhibitiwa na chama cha Democratic limepitisha azimio lisilo na nguvu kisheria la kuweka ukomo katika uwezo wa rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran.


Azimio hilo linamtaka rais Trump kusitisha mipango yote ya kijeshi dhidi ya Iran hadi pale bunge litakapoidhinisha kuingia vitani na nchi hiyo au kuruhusu matumizi ya nguvu za kijeshi kuzuia mashambulizi dhidi ya Marekani. 

Wiki iliyopita rais Trump alitoa idhini ya kumuuwa kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran Qasem Soleimani kisa kilichozusha hasira kutoka kwa Wademocrat na baadhi ya Warepublican waliohoji sababu na uzito wa kufikia uamuzi huo.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema licha ya kwamba azimio hilo halina nguvu kisheria lakini ni ujumbe wa wazi kwa rais Trump kwa sababu linaakisi msimamo wa wabunge.


 Kiongozi wa Republican ndani ya Congress, Kevin McCarthy ameliita azimio hilo kuwa halina maana huku mnadhimu wa chama hicho akilinanga kuwa ni "taarifa kwa vyombo vya habari".

Trump, kupitia ukurasa wake wa Twitter aliwasihi wawikilishi wote wa Republican "wapige kura ya kulikataa azimio hilo la wazimu la Pelosi."


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527