IRAN YARUSHA MAKOMBORA NA KUPIGA KAMBI ZA JESHI LA MAREKANI HUKO IRAQ


Jeshi la Iran (IRGC) limerusha makombora ya balestiki na kupiga kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq, kama jibu la kuuawa  Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha SEPAH.


Taarifa ya IRGC imesema kuwa, Iran imetoa jibu hilo kwa  Marekani alfajiri ya leo, ambapo imelenga uwanja wa ndege wa kijeshi wa Marekani wa Ain al-Assad katika mkoa wa al-Anbar, magharibi mwa Iraq.

Jeshi la Iran limeitaka Marekani iwaondoe wanajeshi wake wote katika nchi hiyo ya Kiarabu, likisisitiza kuwa halitatenganisha kati ya Marekani na Israel katika kujibu mapigo ya kuuawa  Jenerali  wao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad javad Zarif amezungumzia  kuhusu jibu hilo la Iran katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuandika: 



"Iran imechukua hatua madhubuti ya kujihami kwa mujibu wa Sura ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa kulenga kambi ya jeshi ambayo ilitumiwa katika shambulizi la kioga dhidi ya raia na maafisa wetu wa ngazi za juu. Hatutaki kukuza mambo wala vita, lakini tutajihami dhidi ya uvamizi wowote."

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imethibitisha habari hizo za kuvurumishwa makumi ya makombora ya balestiki kuelekea katika kambi  ya jeshi la Marekani nchini Iraq.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527