TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA YASHIRIKISHA WADAU MABORESHO YA SERA


Mkurugenzi wa Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika  Bw. Buji Bampebuye akifungua kikao cha wadau wa Ushirika katika kikao kazi cha kukusanya maoni ya maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika mkoani Dar es salaam, kulia ni Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Abdillahi Mutabazi
Wadau wa Ushirika wakijadiliana kuhusu masuala ya kufanyiwa maboresho katika Sera ya Maendeleo ya Ushirika, mkoani Dar es salaam hivi karibuni
Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara akifungua kikao kazi cha mjadiliano nakupokea maoni ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika Mkoani Mtwara
 
Wadau Mkoani Mtwara wakijadiliana maboresho ya kufanyika katika Sera ya Maendeleo ya Ushirika 


Mkurugenzi wa Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bw. Buji Bampebuye ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Ushirika kutoa maoni yatakayotumika katika kuboresha na kupitia upya Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002. 

Wito huo umetolewa wakati wa ukusanyaji wa maoni hayo katika kikao kazi kilichofanyika Dar es salam hivi karibuni, Tume ilipokutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika pamoja
na wanaushirika waliokuwa wakijadili masuala mbalimbali ya namna bora ya kuboresha utendaji na uendeshaji wa Sekta ya Ushirika nchini. 

“Wana ushirika tujadiliane kwa kina changamoto zilizopo katika Sekta tutoe mapendekezo nini kifanyike na namna gani kifanyike ili kuimarisha na kuondokana na changamoto pamoja na vikwazo vilivyopo katika Sekta ya Ushirika
inayochangia Uchumi wa nchi na kutoa fursa za ajira nchini. 

Ushirika ni wa wanaushirika wenyewe kwa hiyo tumieni fursa hizi vizuri kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa Taifa letu,” alisema Bw. Bampebuye. 

Sambamba na kikao kazi hicho Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara Bw. Juma Mokili akifungua kikao cha wadau katika ukusanyaji wa maoni mkoani Mtwara alisema Sera inatoa Dira ya uendeshaji wa Sekta ya Ushirika.

 Hivyo, wadau wana mchango muhimu katika kuujenga Ushirika watumie fursa hiyo kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru ili kuweka msingi wa Sera bora itakayotumika kuendelea kuunda Sheria, Miongozo pamoja na Kanuni
zitakazotumika kwa maslahi ya wanaushirika na Taifa kwa ujumla. 

Pamoja na mambo mambo mengine wadau walijadili masuala mbalimbali ikiwemo muundo wa Ushirika, fedha, Uwekezaji katika Vyama, Usimamizi na Uendeshaji wa miradi ya Pamoja, mali za Ushirika, ubunifu na Ujasiriamali katika Ushirika, masoko ya bidhaa, huduma za Ushirika,
utawala, usimamizi, utafiti, elimu pamoja na mafunzo ya Ushirika. 

Kwa upande wake Mjumbe wa kikao kazi Mkoani Mtwara Bw.Issa Mangochi kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Masasi na Mtwara (MAMCU) amepongeza utaratibu huo shirikishi ambao umetoa fursa kwa wadau kutoa maoni na mapendekezo yao yatakayosaidia kutengeneza Sera bora zaidi itakayo hudumia wanaushirika wengi zaidi na utendaji wenye tija na maendeleo kwa wananchi. 

Aliongeza kwa kuwaomba watendaji katika Sekta ya Ushirika
kufanya kazi zao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia taratibu za kazi. 

Vikao kazi hivyo vimehusisha wadau kutoka maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Vyama vya Msingi (AMCOS), Vyama vikuu, Taasisi za Vyuo vikuu, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo, Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO).

 Tume tayari imeshapokea maoni kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Kilimanjaro, Kanda ya Juu Kusini mkoani Mbeya pamoja na Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post