WATU NANE WAFARIKI DUNIA BAADA YA KUNYWA POMBE YA MNAZI

 
Watu wanane wamekufa nchini Ufilipino huku wengine zaidi ya 300 wakipelekwa hospitalini baada ya kunywa pombe ya kienyeji maarufu kama mnazi au tembo Afrika Mashariki.

Waliotharika ni watu kutoka miji mbalimbali ambao walinunua kinywaji hicho kinachofahamika na wenyeji kama lambanog katika duka moja, hayo ni kulingana na vyombo vya habari vya eneo.

Watu hao walilalamikia kuumwa na tumbo na kuhisi kisunzi kabla hawajapata matibabu.

Polisi wanasema kwamba idadi kubwa ya waathirika wanatoka mji wa Rizal eneo la Laguna, kusini mashariki mwa mji mkuu Manila. Wengine walitoka mji ulio karibu wa Quezon.

Vyombo vya habari vya ABS na CBN vinasema kwamba mmiliki wa mgahawa unaouza kinywaji hicho cha kienyeji amejiwasilisha kwa maafisa wa polisi.

Kuna taarifa za kutatanisha kuhusu ikiwa mgahawa husika ulikuwa ukiendesha shughuli zake kihalali au kinyume cha sheria.Waathirika wa pombe iliyotiwa sumu wakipata matibabu katika hospitali moja iliyopo Manila

Gavana Ramil Hernandez ameongeza kuwa huenda mamlaka ikaanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

Hii si mara ya kwanza watu kuaga dunia kwa sababu ya kinywa kinywaji hichocha kienyeji huko huko Ufilipino.

Kulingana na taarifa za eneo, karibia watu 21 waliaga dunia mwaka jana baada ya kuywa kinywaji hicho hicho.

Sumu ya methanol inayowekwa kwa kiwango cha juu katika kinywaji hicho ni tatizo kubwa katika sehemu nyingi za vijijini za Asia.

"Ukiuliza watu ikiwa wamewahi kuona sumu ya methanol watasema hapana," Dr Knut Erik Hovda - mtaalam wa kimataifa wa methanol kutoka Chuo Kikuu cha Oslo ameiambia BBC.

"Ukimuuliza mtu huyo huyo ikiwa amewahi kuona mtu akipofuka ama mtu anaaga dunia kwasababu ya sumu hiyo, bila shaka atasema hilo ni jambo linalotokea kila wakati. Na hilo hutokea pale methanol inayotumika kwa kiwango cha juu zaidi kuliko inavyotakikana."

Chanzo- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527