TRUMP ATAMANI KESI YAKE YA KUMUONDOA MADARAKANI IFANYIKE HARAKA


Rais wa Marekani Donald Trump ametaka kesi inayomkabili ya matumizi mabaya ya madaraka  kuwasilishwa katika bunge la seneti mara moja , huku kukiwa na mkwamo miongoni mwa Democrats na Republicans kuhusu siku ya kuanzishwa.

Siku ya Jumatano, bunge la wawakilishi nchini Marekani lilipiga kura ya kutaka kumuondoa madarakani kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka na kulizuia bunge la uwakilishi.

Lakini Democrats wamekataa kuanzisha kesi hiyo ,wakidai kwamba bunge la seneti linadhibitiwa na Republicans ambao wamekataa mashahidi na kwamba haliwezi kufanya kesi ya haki.

Idadi ya wanachama wa bunge la seneti inaonyesha wazi kwamba bwana Trump huenda akaondolewa mashtaka hayo.

Mchakato wa kumuuondoa madarakani rais huyo umechochewa na migawanyiko ya mabunge hao mawili kulingana na vyama vyao.

Mashtaka yaliowasilishwa dhidi ya Trump yanafuatia madai kwamba rais huyo aliishinikiza Ukraine kuchunguza habari kuhusu mpinzani wake wa Democrats Joe Biden na mwanawe wa kiume Hunter, na baadaye akakataa kushirikiana na uchunguzi wa bunge kuhusu swala hilo.

Katika msururu wa jumbe za twitter, Trump aliwashutumu wabunge wa Democrats kwa kukataa kuendelea na kesi hiyo kwa kuwa ''kesi yao ilikuwa mbaya''.

Alituma ujumbe wa twitter akisema; Baada ya Democrats kukataa kunipa haki yangu bungeni, bila kuwa na wakili bila mashahidi, sasa wanataka kuliambia bunge la seneti jinsi ya kuendesha kesi hiyo.

Ili kesi hiyo kuanza, bunge la uwakilishi linalodhibitiwa na Democrats ni sharti liwasilishe nakala za kesi hiyo kwa bunge la seneti.

Lakini spika wa bunge la uwakilishi Nancy Pelosi amekataa kufanya hivyo hadi pale sheria za kesi hiyo za seneti zitakapokubaliwa na Democrats.

Kiongozi wa Republican katika bunge la seneti Mitch McConnell , ataamua masharti ya kesi hiyo na Democrats wanamtaka kutoa maelezo kuhusu mashahidi na ushahidi utakaoruhusiwa.

Bwana McConnel amekataa kukubaliana na Democrats: Tunasalia katika mkwamo, alisema, baada ya mkutano mfupi na kiongozi wa walio wachache wa Democrats Chuck Schumer.

Bwana McConnel ana idadi kubwa ya wabunge wa Republican katika bunge hilo .

Kuna wabunge 53 wa Republican katika bunge hilo lenye viti 100 na kwa kura hiyo kumuondoa madarakani rais Trump itahitaji kuungwa mkono na thuluthi mbili ya wabunge .

-


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post