TANZANIA, KENYA ZAAHIDI KUENDELEZA NA KUKUZA MAENDELEO

Tanzania na Kenya zimeahidi kuendeleza na kushirikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.


Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 56 ya Jamhuri ya Kenya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa Tanzania na Kenya ni ndugu na nchi hizo zitaendelea kushikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya diplomasia ya uchumi baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.

“Sisi Tanzania na Kenya ni ndugu wa damu, kwa hiyo basi tunawatakia sana kila la kheri katika kuiletea Kenya maendeleo…lakini mjue kuwa maendeleo ya Kenya ni maendeleo ya pia ya Tanzania, maendeleo pia ya Uganda, ni maendeleo pia Burundi, maendeleo pia Rwanda na Maendeleo pia ya Sudani Kusini na ni maendeleo pia ya jumuiya ya Afrika Mashariki”. Amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa umoja na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa Kenya na kusema kuwa umoja huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa Tanzania na Kenya.

“Napenda kuwafahamisha kuwa umoja na mshikamano wetu umekuwa chachu ya maendeleo baina ya mataifa haya mawili…..tukumbuke kuwa umoja ni nguvu na dhamira yetu ni kushirikiana na mataifa yote duniani. Na dhamira yetu ni kuishi kwa amani umoja na mshikamano ili kukuza uchumi wetu”. Alisema Balozi Kazungu.

Aidha, Balozi Kazungu amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa ya kipekee kwa taifa la Kenya kutokana na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa nchi ya Kenya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili 2019 Kenya tulipokutana na Tanzania jijini Arusha tuliweza kuondoa vikwazo vya biashara 25 kati ya 37, hii inadhihirisha ni kwa jinsi gani Kenya na Tanzania na ndugu ambao wanapenda kukuza na kuendeleza maendeleo ya biashara”. Ameongeza Balozi Kazungu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527