RAIS WA ZAMANI WA PAKISTAN, PERVEZ MUSHARRAF AHUKUMIWA KIFO

Mkuu wa majeshi wa zamani wa Pakistan ambaye pia alikuwa rais wa nchi hiyo Pervez Musharraf amehukumiwa kifo na mahakama ya kupambana na ugaidi nchini humo baada ya kupatikana na hatia ya uhaini.


Afisa wa sheria wa serikali ya Pakistan Salman Nadeem amevieleza vyombo vya habari kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 6, Musharraf amepatikana na hatia ya kukiuka katiba ya Pakistan.

Kesi ya uhaini dhidi ya Pervez Musharraf, iliyotokana na hatua aliyochukua tarehe 3 Novemba, 2007 ya kutangaza hali ya hatari nchini, ilianza kusikilizwa mwaka 2014.

Kufuatia hatua yake hiyo ya kutangaza hali ya hatari, jenerali huyo mstaafu wa jeshi la Pakistan alisimamisha katiba na kuwaweka kizuizini wanasiasa waandamizi na majaji.

Mgogoro huo ulichochewa na jaribio lililofanywa na Musharraf mnamo mwezi Machi mwaka 2007 la kumwachisha kazi Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu Kabisa ya Pakistan wakati huo Iftikhar Muhammad Chaudhry, uamuzi ambao ulikuja kutenguliwa na kubatilishwa na Mahakama ya Juu Kabisa ya nchi hiyo.

Pervez Musharraf aliingia madarakani mwaka 1999 kupitia mapinduzi ya kijeshi na akaitawala Pakistan kwa muda wa miaka tisa kabla ya kuondolewa uongozini wakati chama chake kiliposhindwa katika uchaguzi mkuu.

Rais huyo wa zamani wa Pakistan ambaye ameelekea uhamishoni yeye mwenyewe huko Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu, aliwahi huko nyuma kukana shtaka hilo la uhaini lililokuwa likimkabili.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Pakistan kwa mtawala wa zamani wa kijeshi kuhukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kufanya uhaini mkubwa.

Wachambuzi wa siasa nchini Pakistan wanasema, hukumu hiyo imeonyesha kuwa hakuna yeyote mwenye kinga ya kutoshtakiwa, na ni ishara pia kwamba Pakistan inabadilika na mfumo wake wa mahakama pia umebadilika.../


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post