NYOKA AUA ASKARI WA WANYAMAPORI KITANDA

Na Yeremias Ngerangera - Namtumbo
Askari msaidizi wa wanyamapori (VGS) wa kijiji cha Kitanda Wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma Halfani Mwale amefariki dunia baada ya kung'atwa na nyoka muda mfupi baada ya tukio hilo.

Tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili ya tarehe 29 Desemba 2019 ambapo marehemu na askari wenzake walikuwa doria katika pori la wanyama la Jumuiya ya Mbarang'andu linalomilikiwa na vijiji kumi vya wilaya ya Namtumbo.

Mtendaji wa kijiji cha kitanda bwana Ayubu Muhuwa alisema marehemu alikutwa na mauti baada ya kukimbizwa kituo cha afya Namtumbo na alipofikishwa kituo cha afya Namtumbo hali haikuwa nzuri na kutakiwa kumfikisha hospitali ya rufaa ya Mkoa Ruvuma na kabla ya kufika hospitali hiyo marehemu alifariki dunia.

Kwa mujibu wa maelezo ya askari mwenzake bwana Rashidi Maramae alidai marehemu amefariki dunia kutokana na kuchelewa kupata huduma ya matibabu kwani eneo alilong'atwa na nyoka haifiki pikipiki wala gari hali iliyowapelekea kumpatia huduma ya kwanza kwa kumfunga kamba na kumbeba kwenye machela mwendo wa masaa manne kwa haraka na kufika eneo linalowezekana kupata usafiri.

Bwana Maramae alisema mara baada ya kufika eneo linalopitika kwa gari walipiga simu kwenye uongozi wa Jumuiya na kutumwa gari ya kumbeba marehemu lakini muda uliotumika toka marehemu alipong'atwa na nyoka saa nane mchana ambapo wao walitembea kwa miguu kumbeba marehemu na kufika eneo linalofika gari ulikuwa muda wa saa 11 jioni na gari ilikuja muda wa takribani saa moja ya usiku hali hiyo ilichelewesha marehemu kupata matibabu alisema Maramae.

Sefu Ndomondo na Joji Nditi askari wasaidizi wa wanyamapori kutoka katika kijiji cha Nambecha walidai kazi hiyo ni ngumu lakini hawapati mshahara wowote na kuongeza kuwa kitendo cha kuona mazingira aliyofia mwenzao wamepata funzo juu ya kazi hiyo.

Askari wasaidizi wa wanyamapori Wilayani Namtumbo wanalalamikia kutolipwa mshahara licha ya kufanya kazi ngumu kuwafukuza wanyama waharibifu na wanaotishia maisha ya jamii katika vijiji vinavyozunguka jumuiya ya Mbarang'andu na kuwafanya wasifanye kazi zao binafsi za kujiongezea kipatao katika familia zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527