NAIBU WAZIRI MABULA AAGIZA WADAIWA NHC KUCHULULIWA HATUA

Na Munir Shemweta WANMM

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekutana na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa saa nne na kulitaka shirika hilo kuhakikisha kufikia Januari 2020 inawachukulia hatua wapangaji wote wa Shirika hilo wanaodaiwa kodi inayofikia bilioni 8.23.

Dkt Mabula alikutana na Menejiment ya Shirika hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam ikiwa ni mkakati wake wa kulifanya Shirika la Nyumba la Taifa kuimarika kimapato pamoja na kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Alisema, katika kuifanya NHC inaimarika kimapato ni lazima madeni kutoka kwa wapangaji wake yanakusanywa kwa kuanzisha opreresheni maalum inatakayowezesha kutambuliwa wadaiwa wote wa kodi ili waweze kulipa kwa wakati.

‘’Ukiacha zile taasisi za serikali, wote wanaodaiwa ikifika januari 2020 wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na zile taasisi za serikali mkamuone Katibu Mkuu HAZINA ili taasisi hizo zikatwe fedha moja kwa moja’’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakati wa zoezi la kufanya opresheni ya kukusanya madeni sheria lazima ifuatwe ikiwemo kutoa hati za wito wa madai kwa wadaiwa wote kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umiliki na Uendelezaji wa Shirika la Nyumba la Taifa Greyson Godfrey alimueleza Dkt Mabula kuwa, pamoja na NHC kuimarika katika makusanyo lakini liko kwenye mikakati maalum wa kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa wake na moja ya jitihada zake ni kuingia makubaliano maalum ya namna wadaiwa watakavyolipa madeni.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Dkt Maulid Banyani alisema Shirika lake limekuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha linaimarika kimapato ikiwemo kutoa motisha kwa watumishi wanaofanya vizuri katika mikoa itakayofikia lengo la makusanyo na  kutokuwa na malimbikizo ya madeni kutoka kwa wadaiwa wa kodi.

‘’Tumekuwa tukitoa motisha kwa watumishi wanaofanya vizuri na sasa tunaangalia ile mikao ambayo haina malimbikizo ya madeni kwa wapangaji wake kwa asilimia mia moja tuone namna tutakavyotoa motisha ili kuhamasisha mikoa kutokuwa na madeni’’ alisema Dkt Banyani

Aidha, Dkt Banyani alisema, kwa sasa NHC imeanza kufanya uhakiki kwa wapangaji wake ili kubaini wapangaji waliopangisha watu wengine ambapo eneo la Ubungo limetumika kama eneo la majaribio  na tayari wapangaji sita washaondolewa na kusisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa ni la nchi nzima.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mabula aliagiza kupatiwa orodha ya nyumba zote za NHC zilizouzwa, zisizouzwa, zilizopangishwa na zisizozopangishwa, viwanja vya Shirika hilo visivyoendelezwa pamoja na Nyumba zilizokuwa za Msajili wa Majumba zilizohamishiwa NHC  hilo ili kujua hali ya shirika na mkakati wake katika kuleta ufanisi.

Pia Dkt Mabula alitembelea maendeleo ya ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo ambao uko katika hatua za mwisho za kukamilika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527