MJUMBE WA KAMATI KUU YA CHAMA CHA KIKOMONISTI CHA CHINA KUZURU TANZANIA


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomonisti cha China (CPC) na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya watu wa China, JI Bingxuan, akiwa na ujumbe wa watu 14 anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe Disemba 17 hadi 19 2019.



Ziara hiyo inafanyika kufuatia mwaliko wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Yustino Ndugai ambaye alifanya ziara ya kikazi nchini China mwezi Julai 2019.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, atakapokuwa nchini, JI atafanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na mwenyeji wake, Spika Ndugai na viongozi waandamizi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) jijini Dar Es Salaam.

Wakati wa ziara hiyo, JI atashiriki hafla ya uzinduzi wa Mpango wa China wa kufufua njia za kale za biashara kati ya Asia na Afrika (Silk Road Community Building Initiative) ili kukuza ushirikiano wa biashara na uchumi baina ya mabara hayo. Mpango huo unaratibiwa na Asasi ya Kukuza Urafiki kati ya China na Tanzania na Asasi dada ya China inayoitwa Chinese Association for International Understanding.

Kabla ya kuhitimisha ziara yake, JI atashuhudia asasi 11 za China zikisaini makubaliano na asasi za kiraia za hapa nchini kwa madhumuni ya kukuza na kuimarisha uhusiano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa faida ya pande zote mbili. 



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527