WAANDISHI NA WATANGAZAJI WA REDIO WAASWA KUZINGATIA WELEDI NA MAADILI YA UANDISHI WA HABARIWaandishi wa habari wanaoripotia redio Jamii (Mtwara), Ruangwa (Lindi), Pambazuko (Ifakara), Chai (Rungwe), Ileje ( Songwe), na Kitulo (Makete-Njombe) wakiwa kwenye kazi za makundi wakijadili namna ya kuandaa habari na kuiwasilisha kwa kutumia miundo mbalimbali ya maudhui.


Waandishi na watangazaji wa Redio za Kijamii nchini wameaswa kuzingatia miiko,maadili na sheria zinazoongoza  taaluma ya habari nchini ili kulinda heshima ya taaluma yao.

Wito huo umetolewa na mjini Morogoro na Mratibu wa mafunzo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi Getrude John wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya waandishi wa habari kutoka redio za kijamii nchini.

Bi Getrude alisema ni vyema waandishi na watangazaji wa redio za kijamii wakatambua wajibu wao ndani ya jamii na hivyo kijibidiisha katika kuielewa taaluma ya habari, misingi, weledi, sheria, mahitaji na matakwa ya wasikilizaji wao pamoja na kuwajua wasikilizaji wao kiasili.

“Ukiwa mwandishi wa habari za kijamii una wajibu mkubwa katika jamii yako na hasa kuhakikisha unaijua jamii yako, hitaji lake pamoja na sheria na maadili ya utangazaji na uandishi wa habari” alisisitiza Bi Getrude.

Alisisitiza kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwa na changamoto nyingi za kiweledi kwenye maudhui ya habari hususani redio za kijamii makosa ambayo waandishi na watangazaji wa redio hizo wana nafasi kubwa ya kuyarekebisha ili kuepuka makosa ya kisheria,kimaadili na kushindwa kutengeneza maudhui yanayotengeneza jamiiyenye mtazamo chanya,yenye ubunifu na inayozingatia maadili ya jamii husika.

“Kazi ya uandishi wa habari ina maadili na sheria zake, ina miiko inayoiongoza,bila kuijua unaweza kujikuta unaingia kwenye mgogoro na jamii unayoihudumia”

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameomba UNESCO kuyaendeleza mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo kutokana na walio wengi kukosa nafasi ya kupata mafunzo ya uandishi wa habari kabla ya kuanza kufanya kazi na redio za kijamii.

“Sisi wengi tunaofanya kazi na Redio za kijamii,hatukubahatika kupitia katika mfumo rasmi wa elimu ya habari, tunaomba tupatiwe mafunzo zaidi ya haya ili tuwe na utaalamu na maarifa yatakayotufanya tuandae maudhui yanayojibu changamoto ya jamii tunazozihudumia huku tukizingatia maadili na sheria” alisema Tumain Obel kutoka Redio Chai FM.

Jumla ya waandishi 24 kutoka redio 6 za kijamii kutoka Tanzania Bara wanahudhuria mafunzo ya siku tano yanayoratibiwa na kuendeshwa na UNESCO chini ya mradi wa SDC yenye lengo la kuwajengea uwezo waandishi na watangazaji wa redio za kijamii kwenye eneo la maadili, sheria, ujuzi na weledi katika taaluma ya habari.

Mafunzo kama haya yalifanyika wiki iliyopita visiwani Zanziar kwa kuhusisha waandishi na watangazaji wa redio za kijamii 16 kutoka vituo 4 vya redio za kijamii kutoka Unguja na Pemba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post