JESHI LA MAGEREZA LASEMA MFUNGWA ALIYEGOMA KUONDOKA GEREZANI ANA MATATIZO YA AKILI


Jeshi la Magereza mkoani Mbeya, limethibitisha kuwa mfungwa Merard Abraham ambaye aligoma kuondoka gerezani baada ya kutolewa kwa msamaha wa Rais John Magufuli wakati wa Sherehe za Uhuru wa Tanzania ana matatizo ya afya ya akili.

Akizungumza na wandishi wa Habari ofsini kwake, Mkuu wa Jeshi la Magereza wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mathias Mkama amesema kijana afya yake ilikuwa inabadilika mara kwa mara.

Amesema pamoja na kwamba alionekana kugoma kuondoka gerezani hapo lakini ndugu zake walienda kumchukua na wakaondoka naye kwenda Mwakaleli wilayani Rungwe na kwamba Jeshi hilo liliwasaidia baadhi ya gharama za usafiri.

Mkama amesema awali alienda ndugu yake mmoja kwa ajili ya kumchukua lakini baada ya kubaini kuwa ni ‘mtata’ akaamua kuwasiliana na ndugu wengine na hivyo wakaja wengi na wakafanikiwa kumchukua.

“Kwa sababu alikuwa amejijeruhi kwa jiwe kwenye paji la uso, tulilazimika kumtibu kwanza kwenye zahanati yetu na baada ya kuchunguzwa matatizo mengine wataalamu wetu walithibitisha kuwa yuko vizuri na hivyo tukaruhusu aondoke,” amesema Mkama.

Amesema wafungwa wote 259 wa walionufaika na Msamaha wa rais walishachukuliwa na ndugu zao na kurejea nyumbani baada ya Jeshi hilo kuwapatia nauli ya kuwarudisha kila mmoja nyumbani kwao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527