CCM YAKARIBISHA MAONI YA MWELEKEO WAKE WA SERA NA ILANI YA UCHAGUZI


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa watanzania na wanachama wa CCM kwamba kiko katika mchakato wa kuandika Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 hadi 2030 pamoja na uaandaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa Mwaka 2020 hadi 2025.


Kama ilivyo desturi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika michakato yake yote ya uaandaji Nyaraka muhimu za Chama ikiwamo Mwelekeo wa Sera na Ilani ya Uchaguzi Msingi Mkuu huwa ni ushiriki na ushikishaji wa umma wa watanzania na wanachama wa CCM kote nchini. Msingi huu wa kushirikisha umma unatokana na asili ya Chama ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ni vitu viwili, kutenda haki na kuheshimu watu.

Chama kinawakaribisha mtu mmoja mmoja au vikundi vya watu na taasisi mbalimbali ikiwemo lakini si kwa uchache, Vyama vya Wafanyakazi, Wawakilishi na vyama vya Wakulima, Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu, Vyama vya Waalimu, Wachimbaji wadogo wadogo wa madini, wafanyabiashara wa madini, wawakilishi na vyama vya wakulima, wavuvi na wafugaji, jumuia za wamachinga na wasafirishaji wadogo wadogo k.v. bodaboda, bajaj n.k., Jumuia za wanawake, watu wenye ulemavu, vijana, wazee, watoto, Asasi Zisizokuwa za Kiserikali (AZISE), wasomi, wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu, wadau na wana tasnia ya Sanaa, burudani na michezo, wasafirishaji wa mizigo na abiria, wenye viwanda, wadau wa sekta ya utalii na vyama vya ushirika kwa maeneo yao.

Kwa wanachama wa CCM Kamati za Siasa za Mikoa na Wilaya ziweke utaratibu wa kukusanya maoni na kuwasilisha Makao Makuu kama ambavyo imekwisha kuelekezwa.

Kamati ya Uandishi wa Mwelekeo wa Sera na Ilani ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Mzee Phillip Japhet Mangula Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara inaomba maoni haya yawe yamefika kwa Kamati kabla ya Tarehe 25 Januari 2020.

§  Maoni yanaweza kuwasilishwa kwa Ndg. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM, Makao Makuu ya CCM, S.L.P 50, Dodoma, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, S.L.P 9151, Dar Es Salaam na Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, Zanzibar, Na kwa baruapepe: katibumkuu@ccm.or.tz

§  Maoni yanaweza pia kuwasilishwa kwa Ndg. Humphrey Polepole, Katibu wa Kamati ya Wataalam kupitia baruapepe: hpolepole@hpolepole.com

Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unapenda kuwatakia wana CCM na Watanzania wote Heri ya Mwaka Mpya, Mwaka 2020 ukawe wenye Baraka, Amani, umoja, neema, mafanikio na kuinuliwa kwa mtu mmoja mmoja na Taifa la Tanzania, sote tukafanye kazi kwa bidii na huu ukiwa ni msingi wa kulinda utu na uhuru wa Taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania na Watu wake,
Mungu Bariki Chama Cha Mapinduzi (CCM) na,
Mungu ubariki Mwaka 2020

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na,


HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527