WAZIRI WA FEDHA DR MPANGO ATOA TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KATIKA MWAKA 2019

Dkt. Philip Mpango (Mb.)
Waziri wa Fedha & Mipango
31 Desemba, 2019 - DODOMA

Ndugu Waandishi wa Habari, Kwanza kabisanapenda nianze taarifa yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye kwa rehema zake ameendelea kutujalia afya njema, amani na utulivu katika nchi yetu katika mwaka mzima wa 2019.


Pili namshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa JMT, kwa kuendelea kuniamini kutumika katika Serikali yake katikanafasi hii nyeti na ngumu ya Waziri wa Fedha na Mipango kwa miaka hii minne (4). Napenda kuwaahidi Watanzania kwamba, kwa msaada wa Mungu, nitaendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kushirikiana na watumishi wenzangu katika Wizara na Serikali nzima, ili kutoa mchango mzuri katika kuijenga Tanzania mpya.

Ndugu Waandishi wa Habari, Ninyi ndiyo kiungo kati ya Serikali na wananchi katika kuwafikishia sera, mipango, mikakati na taarifa mbalimbali kuhusu mafanikio ya Serikali katika kuwapelekea maendeleo na juu ya fursa zilizopo katika sekta binafsi. Ninyi pia ndio mnaoleta mrejesho Serikalini kuhusu maoni, ushauri na dukuduku za wananchi. Vilevile, ninyi mnawakilisha sekta ambayo ni miongoni mwa sekta tano zinazokua kwa viwango vikubwa. Katika mwaka 2018 sekta ya habari na mawasiliano ilikua kwa kiwango cha 9.1% na 10.7% kwa kipindi cha Januari-Juni 2019.Ninawapongeza sana waandishi wa habari wa Tanzania kwa mchango wenu mkubwa katika Taifa letu.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mtakumbuka kwamba Serikali ya awamu ya tanoimetimiza miaka minne (4) kamili tangu ilipoingia madarakani mwezi Novemba 2015. Japo ni kipindi kifupi, watanzania wote wameshuhudia kuwa Serikali yao ya CCM, chini ya uongozi thabiti wa RaisMagufuli, imethubutu kutekeleza mambo mengi makubwa, yakiwemo yale ambayo yalishatolewa uamuzi katika awamu zilizopita lakini hayakutekelezwa. Naomba leo nijikite kuelezea kwa kifupi mwenendo wa uchumi wa Taifa ulivyokuwa katika mwaka huu 2019 unaoisha leo. Aidha, nitatoa tathimini ya awali ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20,  changamoto zilizo mbele yetu na matarajio yetu katika mwaka mpya wa 2020.

1.0 MWENENDO WA UCHUMI WA TAIFA

1.1 Ukuaji wa Pato la Taifa
·       Katika kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo (2016 – 2018) ya utawala wa Rais Magufuli, Uchumi umekua kwa kasi ya wastani wa 6.9%. Mwaka 2018, uchumi ulikua kwa 7.0% ikilinganishwa na 6.8% mwaka 2017 na 6.9% mwaka 2016;
·       Mwaka 2018, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi kwa nchi za SADC, nchi ya pili kwa nchi za EAC; na nchi ya tano kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikitanguliwa na Eritria (12.2%), Rwanda (8.6%), Ethiopia (7.7%) na Ivory Coast (7.4%);
·       Katika kipindi cha Januari–Juni 2019, Pato la Taifa lilikua kwa 6.9% ikilinganishwa na 6.8% katika kipindi kama hicho mwaka 2018.
·       Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa uwekezaji, hasa katika miundombinu kama vile ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege; kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hasa dhahabu & makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo kutokana na hali nzuri ya hewa.
·       Sekta zilizokua kwa kasi kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019 ni pamoja na ujenzi (16.5%), uchimbaji madini na mawe (13.7%), habari na mawasiliano (10.7%), maji (9.1%) na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (9.0%).

1.2 Maana ya Kukua kwa uchumi
Kwa lugha rahisi maana halisi ya kukua kwa uchumi inaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo:
·       Kwanza, ukuaji wa uchumi unaonekana kwa kuangalia ongezeko la uzalishaji (production) kutokana na shughuli za kiuchumi na kiwango cha ushiriki wa wananchi katika shughuli hizo.
ü  Ukuaji wa uchumi ni ongezeko la michango ya shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, viwanda, ujenzi, biashara n.k. na huduma nyingine  ambazo zinafanywa na Watanzania wenyewe kila mwaka.
ü  Kwa ujumla, wanaonufaika na ukuaji kwa kila sekta ni wale wanaoshiriki katika shughuli za sekta husika mmoja mmoja, lakini pia na Taifa kwa ujumla. Huu ndiyo msingi wa msisitizo wa Rais wetu kwamba "kila mtu afanye kazi".
·       Pili, ukuaji wa uchumi katika mwaka husika unaonekana kupitia upatikanaji wa huduma bora zaidi kwa wananchi zilizotolewa na Serikali yao (social impact) ikilinganishwa na ilivyokuwa katika mwaka uliotangulia. Huduma hizo zinajumuisha barabara, elimu, afya, maji, umeme, mitandao ya mawasiliano, na pia ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Huduma hizi zinaokoa gharama (fedha na muda) ambazo wananchi wangetumia kupata huduma hizo. Mathalani:
ü  Kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, gharama za usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda katika masoko zimepungua na vile vile muda wa kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine na gharama za matengenezo ya magari zimepungua.
ü  Upatikanaji wa huduma za jamii kama vile kujengwa kwa vituo vya afya katika kila kata na kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kumepunguza gharama za matibabu kwa wananchi na kumeimarisha afya zao, hivyo kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi za kuinua hali zao za maisha. Ugharamiaji wa elimu-msingi bila ada na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni mojawapo ya matunda ya kukua kwa uchumi.
ü          Huduma za fedha nazo pia zimesogezwa karibu na wananchi kupitia mitandao ya simu na benki mijini na vijijini. Hii imesaidia kuchagiza shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
 1.3 Mfumuko wa Bei
·       Mfumuko wa bei uliendelea kubakia ndani ya lengo la 5.0% katika mwaka ulioishia mwezi Novemba 2019. Katika kipindi hicho, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa 3.8% ukilinganishwa na 3.0% katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Kiwango hiki ni chini ya lengo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki la 8.0%.
·       Nchi nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki nazo zilikuwa na viwango vidogo vya mfumuko wa bei.
ü  Mfumuko wa bei katika kipindi kilichoishia Novemba 2019, kwa Kenya ni asilimia 5.6 na Uganda ilikuwa asilimia 3.0.
·       Mfumuko wa bei wa chakula uliongezeka kufikia wastani wa asilimia 6.7 Novemba 2019, ikilinganishwa na asilimia 2.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Ongezeko hili lilitokana na:
ü  changamoto za usafirishaji, miundombinu ya masoko, maghala  na ugavi wa bidhaa za vyakula kimaeneo; na
ü  uhaba wa vyakula kwa nchi za jirani ambao ulisababisha soko la vyakula kwa nchi hizo kuwa kubwa na kuvutia wafanyabiashara nchini kusafirisha bidhaa za chakula na kuziuza katika nchi hizo.
·       Hata hivyo, ongezeko hili la bei za bidhaa za vyakula linategemewa kuwa la muda mfupi, kwani bado nchi yetu inayo akiba ya kutosha ya chakula (tani 53,000). Pia napenda kutoa wito kwa wananchi hususam wakati huu mvua zipoendelea kunyesha sehemu mbalimbali za Tanzania, tulime mazao ya chakula ya muda mfupi ili kuboresha upatikanaji wa chakula.


1.4 Mwenendo wa Sekta ya Fedha
·       Ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi M3, unaojumuisha sarafu na noti zilizopo katika mzunguko nje ya mabenki na amana katika mabenki ambazo wateja wanaweza kuzichukua wakati wowote wanapozihitaji + fedha zilizoko kwenye amana za muda maalum na amana za akiba +Amana katika fedha za kigeni za wakaazi wa hapa nchini, uliimarika na kuwa wastani wa 11.0% kwa kipindi kilichoishia Oktoba 2019 ukilinganisha na 5.3% kipindi kama hicho mwaka 2018.
·       Ukuaji huu ulikuwa sawia na mahitaji ya uchumi baada kuongezeka kwa kasi ya mzunguko wa fedha kutokana na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya malipo.
·       Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi nao uliendelea kukua kwa wastani wa 9.8% Oktoba 2019 ukilinganisha na wastani wa 4.8% kwa kipindi hicho mwaka 2018.

1.5 Mwenendo wa Biashara ya Bidhaa na Huduma Nje
·       Katika kipindi cha mwaka ulioishia Oktoba 2019, nakisi ya urari wa biashara na huduma ilipungua hadi kufikia dola za Marekani milioni 126.8 kutoka dola za Marekani milioni 882.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.
·       Kupungua huko kulitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje na mapato ya huduma. Katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2019, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma iliongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 3,639.6, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 2,771.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 31.3. Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa zilizouzwa nje hususan korosho na dhahabu.
·       Aidha, katika kipindi hicho pia, thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje iliongezeka kwa kasi ndogo ya asilimia 3.1 na kufikia dola za Marekani milioni 3,766.4 kutoka dola za Marekani milioni 3,654.6 mwaka 2018/19.
·       Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,395.07 mwezi Oktoba 2019,  ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 5,277.85 mwezi Oktoba 2018. Kiasi hicho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi 6.1. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la kukidhi miezi 4.0, zaidi ya lengo la miezi 4.5 na miezi 6.0 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika, kwa mtiririko huo.

1.6 Thamani ya Shilingi ya Tanzania
ü    Thamani ya Shilingi imeendelea kuwa tulivu. Tangu Julai hadi Novemba 2019, USD.1 ilibadilishwa kwa wastani wa Tshs. 2,291, ikilinganishwa na Tshs. 2,276 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Maana yake, thamani ya shilingi ilipungua (depreciation) kwa 0.6% tu kwa kipindi hicho; Utulivu huo wa thamani ya shilingi umetokana na: Utekelezaji madhubuti wa Sera ya Fedha; Usimamizi imara wa mapato & matumizi; na Mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini.

1.7 Mwenendo wa Sekta ya Benki
·       Sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye kutengeneza faida, ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha zaidi ya kiwango kinachotakiwa kisheria.
·       Uwiano wa mitaji ya mabenki ikilinganishwa na rasilimali zao ulikuwa 16.23% Juni 2019, ikiwa juu ya kiwango kinachohitajika kisheria cha 10.0%.
·       Kiwango cha mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu ikilinganishwa na kiwango cha amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi kilifikia 34.81% ikilinganishwa na kiwango cha chini kinachohitajika kisheria cha 20%.
·       Hii inaashiria kuwa mabenki yana ukwasi wa kutosha kwa ajili ya shughuli zake za kila siku ikiwemo kulipa madeni pamoja na kutoa mikopo.
·       Katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2019, faida ya benki itokanayo na mali (return on assets -ROA) ilifikia wastani wa asilimia 1.85 huku faida ya benki itokanayo na mtaji (return on equity- ROE) ilifikia wastani wa asilimia 7.79.
·       Uwiano wa mikopo chechefu uliongezeka hadi kufikia 10.8% ya mikopo yote Oktoba 2019 kutoka 9.7% kipindi kama hicho 2018. Kiwango hiki ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango cha wastani wa asilimia 5.0 ya mikopo chechefu kinachokubalika kwa mujibu wa sheria.
·       Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto hiyo. Hatua hizo ni pamoja na kuyataka mabenki:
ü  kutekeleza mikakati ya kuboresha utoaji na usimamizi wa mikopo, ikiwemo uchambuzi wa maombi ya mikopo, na kutumia kwa lazima taarifa ya historia za wakopaji (Credit Reference Bureau) kabla ya kutoa mkopo wowote; na kuanzisha idara maalum ya kufuatilia ukusanyaji wa madeni.

1.8 Deni la Serikali
·       Hadi tarehe 30 Novemba 2019, deni la Serikali lilifikia Tshs. 54.84 sawa na ongezeko la asilimia 11.7 ikilinganishwa na Tshs. trilioni 49.08 Novemba 2018.
·       Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Tshs. trilioni 40.39 na deni la ndani ni Tshs. trilioni 14.44. 
·       Ongezeko la deni hilo limetokana na:
ü  Riba ya mikopo ambayo mikataba yake iliingiwa zamani; na
ü  Mikopo mipya, yenye masharti nafuu na ya kibiashara, kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
·       Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa fedha tulizokopwa zinatumika kujenga rasilimali ambazo ni msingi wa kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mali na kuendeleza Taifa lakini pia uwezo wa kulipa mikopo hiyo. Mikopo hii imetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo: ujenzi wa miondombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege; ujenzi wa mitambo ya kufua umeme; na utekelezaji wa miradi ya maji.

1.9 Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Serikali
·       Matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanywa Desemba 2018, inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia vigezo muhimu vinavyotumika kimataifa:
ü  Uwiano wa deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni 27.2% ikilinganishwa na ukomo wa 70%;
ü  Uwiano wa deni la nje pekee kwa Pato la Taifa ni 22.2% (ukomo ni 55%);
ü  Uwiano wa deni la nje kwa mauzo ya nje ni 157.3% (ukomo ni 240%);
ü  Ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni 15.2% ikilinganishwa na ukomo wa 23%.
·       Hii ina maana kuwa Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa toka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje kwa wakati.
·       Mwezi huu wa Desemba 2019, Serikali pia imefanya tathmini hiyo na matokeo ya awali hayatofautiani sana na tathmini ya mwaka jana (Desemba 2018). Matokeo rasmi ya tathmini mpya yatatolewa baada ya uchambuzi unaendelea kukamilika.

1.10 Mapato ya Ndani
·       Mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2019, yalifikia shilingi bilioni 8,501.4 sawa na asilimia 94.4 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 9,010.2 katika kipindi hicho.
·       Kati ya hayo:
ü  Mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 7,179.2 sawa na asilimia 95.5 ya makadirio ya kipindi hicho ya shilingi bilioni 7,514.4;
ü  Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 1,012.8 ikiwa ni asilimia 86.5 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,170.3;
ü  Makusanyo ya mapato kutoka katika Taasisi na Mashirika ya umma kwa mwaka 2018/19 yalikuwa Shilingi Trilioni 1.053 kutoka katika Taasisi na Mashirika 79 hadi kufikia siku ya kuwasilisha gawio kwa Mhe. Rais tarehe 24 Novemba, 2019. Mashirika yaliyochangia ni 79 kati ya Mashirika 266 yaliyopo. Hivyo, kuwa na Mashirika 187 ambayo hayakuwasilisha gawio na Michango katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Kuanzia tarehe 25 Novemba, 2019 hadi tarehe 30 Desemba, 2019 jumla ya Mashirika 137 yamewasilisha michango yao kutekeleza agizo la Mhe. Rais kwa kuchangia kiasi cha Shilingi bilioni 19.6. Hadi sasa bado Mashirika na Kampuni 50 ambazo hazijachangia na narudia kusisitiza kuwa wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi husika watekeleze maelekezo ya Mhe. Rais la sivyo waondoke kwenye nafasi zao ifikapo saa 6 kamili usiku tarehe 23 Januari 2020. Hadi kufikia tarehe 30 Desemba, 2019 jumla ya kiasi cha shilingi trilioni 1.072 zimekusanywa ikilinganishwa na shilingi bilioni 673.502 zilizokusanywa kutoka katika Taasisi na Mashirika ya umma 46 mwaka 2017/18. Nataoa pongezi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa usimamizi mzuri wa taasisi na mashirika ya umma uliopelekea mafanikio haya.

ü  Mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni shilingi bilioni 309.4 ikiwa ni asilimia 95.0 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 325.6.
·       Mwezi Septemba 2019, mapato ya kodi yalivunja rekodi ya makusanyo tangu tupate uhuru, baada ya kukusanya Tshs. Trilioni 1.7. Natoa pongezi nyingi kwa TRA.
·       Pamoja na kwamba mapato ya ndani kwa ujumla yaliongezeka ukilinganisha na kipindi kama hiki mwaka uliotangulia, kiasi kilichopatikana ni pungufu ya lengo lililokusudiwa kwa asilimia 5.6 na sababu kubwa ikiwa ni ukwepaji wa kodi

1.11 Misaada na Mikopo Nafuu
·       Katika mwaka 2019/20, Washirika wa Maendeleo waliahidi kuchangia katika bajeti ya Serikali shilingi bilioni 2,783.3 Hadi kufikia Novemba, 2019, kiasi cha shilingi bilioni 1,115.5 kimepokelewa, sawa na asilimia 8.4 zaidi ya lengo la kipindi hicho.
·       Sehemu kubwa ya fedha zilizopokelewa zilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambazo zilipelekwa moja kwa moja kwenye sekta zinazotekeleza miradi hiyo na hakukuwa na fedha zilizopokelewa kwa ajili ya misaada na mikopo ya kibajeti
1.12 Mwenendo wa Matumizi ya Serikali
·       Kama mnavyokumbuka, bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, iliyoidhinishiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa shilingi bilioni 33,105.4. Kiasi hicho kinajumuisha:
ü  Shilingi bilioni 20,856.8 kwa ajili ya matumizi ya kawaida; na
ü  Shilingi bilioni 12,248.6 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
·       Katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2019,
ü  Matumizi ya kawaida yalifikia Tshs. bilioni 8,708.4 (97.8% ya lengo); na
ü  Matumizi ya maendeleo yalifikia Ths. bilioni 3,150.9, sawa na 61.7% ya lengo;
·       Fedha za matumizi ya maendeleo zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali:
ü  Ujenzi wa SGR ambao kwa sasa umefikia 70% kwa sehemu ya Dar es Salaam – Morogoro (km 300) na 20% sehemu ya Morogoro – Makutupora (km 422);
ü  Ujenzi wa Mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere;
ü  Ujenzi wa barabara na madaraja ikiwemo Ubungo Interchangeambayo ujenzi wake umefikia 55%; daraja la Selander (12%); barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (asilimia 41%); na ujenzi wa barabara za lami katika maeneo mbalimbali nchini unaoendelea;
ü  Ugharamiaji wa miradi ya kimkakati 22 ya kuongeza mapato na kupunguza utegemezi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa;
ü  Miradi ya Maji ya Kitaifa;
ü  Kupeleka umeme vijijini kupitia REA; na
ü  Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania.
·       Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha ni pamoja na:
ü  Ulipaji wa deni la Serikali;
ü  Mishahara ya watumishi;
ü  Utekelezaji wa miradi ya miundombinu (barabara, reli, nishati);
ü  Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na elimumsingi bila ada;
ü Miradi ya maji mijini na vijijini; na
ü Huduma za afya (dawa, miundombinu, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba) 


2.0 MATARAJIO HADI JUNI 2020
·       Pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 mwaka 2019 na kwa wastani wa asilimia 7.1 katika kipindi cha muda wa kati. Maoteo hayo yamejengwa katika misingi ya:
ü  Uendelezaji wa uwekezaji katika miradi ya miundombinu,
ü  Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara; na
ü  Azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda.
·       Kulingana na hatua iliyofikiwa hadi nusu ya kwanza ya mwaka 2019 ya ukuaji wa asilimia 6.9 pamoja mwenendo mzuri wa viashiria vingine vya uchumi, ni dhahiri kuwa lengo la mwaka la 7.0% litafikiwa.
·       Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja chini ya 5% hadi Juni 2020.
·       Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi unatarajiwa kuendelea kuongezeka kufuatia hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali, ikiwamo kuboresha masoko ya fedha, utendaji wa mabenki, mazingira ya kufanya biashara na upatikanaji wa taarifa za wakopaji.
·       Kuhusu upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti kama ilivyoidhinishwa, mapato yaliyopatikana kutoka vyanzo vyote hadi sasa (Novemba) ni asilimia 98.5 ya makadirio. Hivyo matarajio ya Serikali ni kwamba malengo ya mwaka yatafikiwa.
·       Kuhusu matumizi katika kipindi kilichobaki hadi Juni 2020, Serikali itaendelea kuwianisha mapato na matumizi ikiwa ni pamoja na kutoa kipaumbele kwa mahitaji yasiyoepukika kama vile deni la Taifa, mishahara ya watumishi, uendeshaji wa ofisi na utekelezaji wa miradi muhimu yenye maslahi mapana kwa Taifa.

3.0 BAADHI YA CHANGAMOTO 
·       Pamoja na mafanikio niliyoyataja na matarajio mazuri ya mwelekeo wa uchumi na bajeti, zipo changamoto mbalimbali ambazo Serikali inaendelea kukabiliana nazo kwa kushirikiana na wadau hususan sekta binafsi.
·       Baadhi ya changamoto hizo ni kama ifuatavyo;
ü  Uwezekano wa kupanda kwa bei za mafuta kwenye soko la dunia. Serikali inaendelea na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na gesi asilia pamoja na ujenzi wa bwawa/mtambo wa kufua umeme utokanao na nguvu za maji katika bonde la Mto Rufiji.
ü  Athari za Vita vya kiuchumi baina ya mataifa makubwa kiuchumi (hususan Marekani na China) na athari kwa bei ya bidhaa na huduma za nchi yetu katika nchi hizo. Serikali inatekeleza mikakati ya kuongeza wigo wa washirika wa biashara na uwekezaji (ikiwemo utalii) hususan katika nchi zinazoibukia kiuchumi.
ü  Kuongezeka kwa gharama za mikopo kwenye masoko ya fedha duniani kutokana na sera za nchi kubwa kiuchumi (hususan Marekani na nchi za Ulaya). Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha mapato ya ndani na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha. Aidha, juhudi zinaendelea kupata vyanzo vingine vya mikopo ya nje vyenye riba nafuu na kuimarisha uhamasishaji wa wadau katika soko la ndani kwa lengo la kuimarisha ushiriki wao katika minada ya dhamana za Serikali.
ü  Mabadiliko ya hali ya hewa hasa kwa upande wa kilimo ambapo sehemu kubwa bado inategemea mvua. Serikali inatekeleza mikakati ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuhifadhi vyanzo vya maji.

4.0 HITIMISHO
Ndugu Waandishi wa Habari, Naomba sasa mniruhusu nihitimishe taarifa yangu kwenu na watanzania wote kwa kuelezea kwa kifupi mambo sita (6) muhimu:

4.1 Wahujumu Uchumi Wanaotengeneza na Kusambaza Noti Bandia
Ndugu Waandishi wa Habari, siku za karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vimeweza kubaini na kukamata wahujumu uchumi wanaotengeneza na kusambaza noti bandia. Hili ni kosa kubwa kisheria na wananchi wanatahadharishwa kuwa makini wanapokuwa wanapokea fedha hata kama ni za zawadi. Kitu muhimu cha kuzingatia ni kutambua alama za usalama kwenye fedha zetu ambapo Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania na vyombo vya habari, itaendelea kutoa elimu ya utambuzi wa alama za usalama zilizopo kwenye noti halali ili kuwawezesha wananchi kuweza kutambua noti bandia kwa urahisi na namna ya kutoa taarifa ya uwepo wa fedha bandia.

Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa niaba ya Serikali napenda kuwapongeza sana viongozi, watendaji na maafisa wa Benki Kuu ya Tanzania, Vyombo na vyote vya Ulinzi na Usalama, taasisi na wananchi wazalendo waliotuletea taarifa muhimu, ambao kwa pamoja waliiwezesha Serikali kuwafuatilia kimyakimya na hatimaye kuwatia mbaroni wahalifu hao. Aidha, napenda nitambue hadharani mchango mzuri sana wa viongozi wachache katika zoezi hilo akiwemo Mhe. Ole-Sabaya, Mkuu wa Wilaya ya Hai na Mhe. Col. Anange Simon, Mkuu wa wilaya ya Kasulu. Nataka kusisitiza hapa kuwa Serikali itaendelea kuwasaka, kufuatilia nyendo na mitandao yao yote, kuwakamata na kuwachukulia hatua kali sana wale wanaojihusisha na uhalifu huu kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu uchumi ya Mwaka 1984 (The Economic and Organized Crime Control Act, 1984), ikijumuisha hata wale watakaokutwa na hizo fedha bandia. Hivyo, ninawatahadharisha wananchi wote, mabenki yote, na wale wanaotoa huduma za kutuma au kupokea fedha kupitia simu za kiganjani (M-pesa, Tigo-pesa, Airtel money, Halo-pesa, T-pesa na Easy pesa) kuwa makini sana na pia wawe wepesi wa kutoa taarifa kuhusu watu wanaotengeneza na wanaosambaza fedha bandia ili watiwe nguvuni na kupata cha moto wa volkano! Serikali hii haitakuwa na huruma hata kidogo na wahalifu hao!

4.2 Riba Kubwa Zinazotozwa na Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha
Ndugu Waandishi wa Habari, Jambo la pili ni kuhusu adha na dhuluma kwa wananchi wengi wa kipato cha chini na wastaafu kutokana na viwango vikubwa vya riba za kati ya 36% mpaka 240% kwa mwaka vinavyotozwa na taasisi za huduma ndogo za fedha. Baadhi ya changamoto ni kukosekana kwa uwazi na masharti ya mikopo hiyo, mikopo hiyo kutolewa kiholela na kusababisha malimbikizo ya madeni kwa wateja, baadhi ya taasisi hizo hazitoi gawio au faida kwa wananchama au wateja, ukusanyaji wa madeni kwa njia zisizofaa unaosababisha wananchi kunyang'anywa mali zao, na baadhi ya taasisi hizo kuwa upenyo wa utakatishaji wa fedha haramu. Tarehe 13 Desemba nilizindua Mpango wa Elimu kwa Umma Kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za huduma ndogo za Fedha hapa Dodoma. Zoezi hili ni endelevu na lengo la Serikali ni kuwapa wananchi uelewa wa pamoja kuhusu Sera (2017) na mambo muhimu yaliyowekwa katika Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha (2018) ikiwa ni pamoja na mamlaka Benki Kuu ya Tanzania kusimamia sekta ndogo ya fedha, masharti ya kuwalinda watumiaji wa huduma ndogo za fedha, utaratibu wa kusimamia utoaji wa riba na gawio kwenye hisa, akiba na amana zinazokusanywa na taasisi za huduma ndogo za fedha, na makosa na adhabu zitakazotolewa kwa kukiuka masharti yaliyowekwa. Nawaomba wananchi wachangamkie mafunzo hayo ya elimu kwa umma ambayo yamepangwa kuendeshwa nchi nzima kikanda. Aidha, Nachukua tena fursa hii kukemea vikali taasisi ndogo za fedha zinazo endeleza taratibu dhalimu za ukusanyaji wa malipo ya mikopo kutoka kwa wananchi wanyonge kinyume cha sheria. Ninaiagiza tena Benki Kuu ya Tanzania kuongeza nguvu katika kufuatilia mwenendo wa taasisi zote zinazotoa huduma ndogo ya fedha nchini. Aidha, BoT izichukulie hatua kali za kisheria taasisi zote zitakazobainika kuvunja sheria.

4.3 Madai kwamba Serikali Imebana Pesa
Ndugu Waandishi wa Habari, Jambo la tatu ni kuhusu madai kwamba Serikali imebana pesa. Napenda kusisitiza kuwa Serikali haigawi pesa kwa wananchi, badala yake, Serikali inaingiza pesa kwenye uchumi kwa njia kuu zifuatazo: (i) kupunguza kodi, kuongeza matumizi ya serikali (expansionary fiscal policies) au/na (ii) kuongeza ujazi wa fedha, kushusha riba, na kushusha thamani ya shilingi (expansionary monetary policies). Endapo Serikali itaona ni vema kupunguza pesa kwenye uchumi inatumia njia kinyume na hizo nilizozitaja (contractionary fiscal and/or monetary policies).

Ndugu Waandishi wa Habari, Kama nilivyokwisha eleza, Kwa upande wa hatua za kibajeti, Serikali ya awamu ya tano imefanya jitihada kubwa kupunguza viwango na utitiri wa kodi na tozo mbalimbali ambapo kwa mwaka wa fedha 2019/20 Serikali ilifuta au kupunguza ada na tozo 54. Pia matumizi halisi ya Serikali yameendelea kuongezeka kutoka Tshs. trilioni 22.5 (2015/16), Tshs. trilioni 25.4 (2016/17), Tshs. trilioni 26.6 (2017/18) hadi Tshs. trilioni 27.0 (2018/19). Vilevile Serikali imeendelea kulipa madai mbalimbali yaliyohakikiwa ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi mwezi Novemba 2019, Serikali imelipa jumla ya Tshs. trilioni 2.599. Kati ya hizo, watumishi walilipwa Tshs. bilioni 225.07, wazabuni Tshs. bilioni 443.90, watoa huduma Tshs. bilioni 172.84, wakandarasi Tshs. trilioni 1.67 na madai mengineyo Tshs. bilioni 84.45. Aidha, Serikali imeendelea kufanya jitihada kuhakikisha kwamba miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa hapa nchini inatumia kwa kadri inavyowezekana malighafi na bidhaa (saruji, mabomba, bidhaa za chakula, nguzo za umeme n.k) zinazopatikana hapa nchini na kutoa kipaumbele kwa ajira za watanzania katika miradi hiyo. Kwa upande wa mwenendo wa sekta ya fedha, awali nilieleza kuwa ujazi wa fedha umeendelea kuongezeka kwa kuwianishwa na mahitaji ya uchumi. Kasi ya mzunguko wa fedha nayo imeongezeka kutokana na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya malipo, ikiwemo simu za mkononi. Vilevile, riba za mikopo zimeshuka japo kwa kiasi kidogo na thamani ya shilingi imaendelea kuwa imara. Pia, ukwasi katika mabenki ni wa kutosha kabisa na ukuaji wa mikopo ya mabenki kwa sekta binafsi nao umeendelea kuongezeka. Kwa ufafanuzi huo, ni dhahiri kuwa, madai ya baadhi ya watu kuwa Serikali imebana pesa hayana ukweli kwa kuwa milango ya Serikali kuingiza fedha kwenye uchumi iko wazi na takwimu zinathibitisha kuwa uchumi unakua na Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikiongeza pesa kwenye uchumi. Ndiyo maana kwa mfano tunaona nyumba bora zinaendelea kujengwa mijini na vijijini, ununuzi wa magari binafsi na pikipiki unaongezeka, matumizi ya walaji (consumer spending) yanaongezeka, sehemu za starehe mijini na vijijini hazipungui wateja, umiliki na matumizi ya simu za mkononi nayo pia yameongezeka na hata michango ya harusi sioni ikipungua! Lakini, jambo la kweli kabisa ni kuwa Serikali imedhibiti kwa kiasi kikubwa milango ya ukwepaji kodi, biashara haramu ya madawa ya kulevya na utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya ya fedha za umma, madai hewa, rushwa na ufisadi. Napenda nisisitize kuwa milango hiyo ya nyuma ya kuingiza fedha kwenye uchumi imefungwa na Serikali ya Rais Magufuli haina mpango wa kuifungua tena!! Tutaendelea kubana kwa kufuli la titanium (strongest metal) fedha zote zilizokuwa zinapita milango hiyo haramu!!  

Ndugu Waandishi wa Habari, Kumekuwapo pia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara kuwa mwenendo wa biashara zao umeendelea kuwa mgumu na biashara haziendi kutokana na gharama kubwa za kodi na pango. Aidha, ugumu wa biashara unahusishwa na madai niliyoeleza kwamba Serikali imebana pesa lakini pia kwamba bado kuna utitiri wa kodi na tozo, viwango vikubwa vya kodi visivyo na uhalisia na kuongezeka kwa kodi ya pango katika maeneo ya biashara. Taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2019 zinabainisha mwenendo tofauti tofauti wa biashara kutegemea na aina ya biashara lakini kwa ujumla biashara iliongezeka. Kwa mfano, kwa upande wa shughuli za biashara za uuzaji na ununuzi wa bidhaa wa jumla na rejareja pamoja na ukarabati wa magari na wa bidhaa za nyumbani ziliongezeka kwa kiwango cha 5.4% ikilinganishwa na 5.1% kwa kipindi kama hicho mwaka 2018. Shughuli za fedha na bima ziliongezeka kwa kiwango cha 4.7% ikilinganishwa na kiwango cha -0.5. mwaka 2018. Hata hivyo, kwa baadhi ya biashara, ikiwemo huduma za makazi ya muda mfupi kwa wageni/wasafiri na huduma ya chakula na vinywaji  ziliongezeka kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na ukuaji ulivyokua mwaka 2018.

Ndugu Waandishi wa Habari, Ni ukweli ulio wazi kuwa Serikali ya awamu ya tano imechukua hatua za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini ikiwa pamoja na kufuta kodi na tozo nyingi za kero kuliko awamu zote zilizotangualia na pia kutoa ahueni kwa walipa kodi waliokuwa na malimbikizo ya nyuma ya riba na adhabu (tax amnesty on interest & penalties). Aidha Serikali iliandaa na inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment) kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini. Serikali pia imezuia watumishi wa TRA kuwafungia biashara na badala yake watatue matatizo ya wafanya biashara kwa njia ya majadiliano na hata kuwaruhusu kulipa malimbikizo ya kodi kwa awamu.

Ndugu Waandishi wa Habari, Pamoja na hatua zote hizo, naomba nitumie fursa hii kuwatangazia wafanya biashara na wananchi wote kuwa kwa kipindi cha miezi miwili (Januari - Februari 2020) Wizara ya Fedha na Mipango inakaribisha maoni na ushauri kuhusu changamoto zote wanazoona zinakwamisha biashara hapa nchini. Aidha Wizara yangu itaanda mikutano ya ana kwa ana na baadhi ya makundi ya wafanya biashara kupokea maoni na ushauri wao wa jumla na wa kisekta. Ninawaahidi kuwa hoja na ushauri utakaowasilishwa tutaufanyia kazi kikamilifu ili kuchochea biashara kwa manufaa ya nchi yetu. Nawasihi watanzania wenzangu kutumia fursa hiyo kikamilifu.


4.4 Kasoro na Udanganyifu Katika Utoaji wa Risiti za EFD
Ndugu Waandishi wa Habari, Jambo la nne ni kuhusu matumizi ya risiti za risiti za EFD (electronic fiscal devices). Nianze kwa kuwapongeza wafanya biashara wote ambao wanatumia mashine za EFD kwa uadilifu wanapofanya biashara zao.  Hata hivyo, bado kuna kasoro na udanganyifu hususan katika utoaji wa risiti hizo unaofanyika kwa makusudi ili kukwepa kulipa kodi stahiki. Baadhi ya wafanyabiashara bado wauza bidhaa zao kwa bei mbili, moja inakuwa ni bei kubwa zaidi pale mnunuzi anapotaka apatiwe risiti ya EFD na nyingine ni bei ya chini kama mteja yuko tayari kununua bidhaa husika bila kupatiwa risiti ya EFD! Aidha, wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao wamechezea mashine za EFD na risiti wanazotoa hazioneshi kiasi halisi cha fedha zilizolipwa na mteja! Wengine pia wanatoa risiti za EFD zenye tarehe tofauti na tarehe ya siku manunuzi yanapofanyika! Wapo pia wafanyabiashara wanaosingizia mitandao hata pale ambapo duka jirani mtandao uleule upo! Wapo pia wachache wanaharibu mashine hizo kwa makusudi ili zisifanye kazi na wapo wengine ambao wanatoa taarifa za uongo kuhusu kiwango cha mauzo yao ili kukwepa kuingia kwenye kundi la wafanya biashara wanaostahili kuandikishwa (VAT registered). Kama hiyo haitoshi, wapo wafanyabiashara ambao hawatumii kabisa mashine za EFD mpaka pale wanapojua kwamba TRA wanaendesha msako kuwabaini wafanyabiashara ambao hawatumii mashine za EFD! Vilevile, bado wananchi wengi hawaoni umuhimu wa kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa au huduma. Narudia tena kuwakumbusha na kuwaasa wafanyabiashara kutoa risiti za EFD sahihi wakati wote wanapouza bidhaa au kutoa huduma na wananchi nao wadai risiti za EFD na wazikague pale wanaponunua bidhaa au huduma. Naowaomba wananchi wenzangu tuzingatie hili maana kushindwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na TRA ikikubaini utapata adhabu kwa mujibu wa sheria. Lakini lazima tutambue kwamba kwa kukwepa kodi tunajipa adhabu kubwa sisi wenyewe na watanzania wote kwa kuwa tunakuwa tunajicheleweshea kupata huduma bora za afya, elimu na maji na  miundombinu kama barabara na umeme.

Ndugu Waandishi wa Habari, Hata hivyo, napenda kuwakumbusha kwa mara nyingine tena watumishi wa TRA kuwa hairuhusiwi kufunga biashara yeyote isipokuwa kwa idhini ya Kamishna Mkuu wa TRA. Ninawataka maafisa wa TRA kuwa makini katika ukadiriaji wa kodi kwa wafanyabiashara na hilo lifanyike kitaalam, kiuhalisia na kwa kutenda haki. Nataka unyanyasaji wa wafanyabiashara au uonevu katika ukadiriaji wa kodi uliokuwa unafanywa na baadhi ya maafisa wa TRA kwa maslahi binafsi ikiwa pamoja na kudai rushwa, yote yasijirudie. Ninataka TRA ambayo ni safi na rafiki wa wafanyabiashara. Aidha, ninawakumbusha pia kusikiliza na kuelewa changamoto za wafanyabiashara na kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya matakwa ya sheria za kodi. Nina imani kubwa na Kamishna Mkuu wa TRA na kwamba atasimamia maelekezo haya kikamilifu.

4.5 Ulipaji wa Kodi ya Majengo
Ndugu Waandishi wa Habari, Jambo la tano, ni kuhusu ulipaji wa kodi za majengo. Naomba kupitia kwenu wanahabari niwakumbushe watanzania wenzangu kulipa kodi ya majengo wanayoyamiliki na ilipwe mapema bila kusubiri mwisho wa mwezi Juni na hivyo kuepuka asumbufu na adha ya misururu mirefu kwenda kulipa kodi ya majengo. Ninawasihi viongozi wote kuwa mfano bora wa kulipa kodi ya majengo. Usisubiri mpaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikubaini kwamba hata wewe kiongozi hulipi kodi ya majengo!! Natamani miaka ijayo Kamishna wa Maadili ataanzisha utaratibu wa kutudai sisi viongozi stakabadhi za kulipia kodi ya majengo tunayomiliki!! Serikali imeweka viwango vidogo vya kodi ya majengo ili kila mwenye jengo aone wepesi na umuhimu wa kuchangia maendeleo ya Taifa. Katika maeneo ya halmashauri za majiji, miji na manispaa ni Tshs. 10,000 kwa nyumba ya kawaida na Tshs. 50,000 kwa kila ghorofa ya ghorofa. Kwa upande wa halmashauri za wilaya viwango vya kodi ya majengo ni  Tshs. 10,000 kwa nyumba ya kawaida na Tshs. 20,000 kwa kila ghorofa. Natoa rai kwa wananchi wote tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi zilizowekwa kisheria, ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo, ili hatimaye kama Taifa letu liondokane na utegemezi wa kiuchumi.

4.6 Pongezi kwa Wananchi wanaohamasisha Ulipaji Kodi kwa Ubunifu
Ndugu Waandishi wa Habari, Jambo la sita na la mwisho, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa baadhi ya Watanzania ambao wanatumia muda wao katika maeneo ya shughuli zao kuhamasisha wateja au waumini wao kulipa kodi na kudai risiti wakati wanaponunua bidhaa au kupata huduma yoyote hapa nchini. Kuna mifano michache ninayoweza kuishuhudia hapa ikiwa ni pamoja na Mhubiri maarufu Mchungaji Daniel Mgogo ambaye ameweza kutumia muda na karama yake ya kichungaji katika mahubiri kanisani kuhamasisha wananchi kulipa kodi na kudai risiti wakati wa kununua bidhaa na huduma. Vile vile, bila shaka wengi mtakuwa mmeshuhudia clip iliyozunguka mtandaoni ikimwonesha kondakta mmoja katika basi lililokuwa linaelekea Arusha (bahati mbaya sijafanikiwa kupata jina lake na kama akisikia taarifa hii anitumie jina lake kwa ujumbe mfupi kwenye namba ya simu yangu ya mkononi 0787-570714) akiwahamasisha abiria wake kudai risiti wakati basi hilo linaposimama kwa ajili ya huduma ya chakula. Hizi ni baadhi ya juhudi za watanzania wachache ambao kama tutaiga mfano wao mzuri na wa kizalendo itatuwezesha kwa pamoja kujenga nchi yetu na kuboresha maisha ya wananchi wetu, hasa wanyonge, kwa kuwa kodi stahiki italipwa Serikalini na hivyo kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa jamii. Kwa niaba ya Serikali niwashukuru na kuwapongeza sana wote wawili Mchungaji Daniel Mgogo na yule kondakta wa basi na pia wengine wote ambao labda sijapata tu fursa ya kuwasikia, kwa mchango huo mzuri wa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa maendeleo ya Tanzania. Ninawaomba watanzania wakereketwa wa maendeleo na makundi mbalimbali ya jamii hususan wasanii, wana muziki, kwaya, wafanyabiashara bila kuwasahau wana habari, watumie tasnia zao na ubunifu kuunga mkono jitihada hizo za kuhimiza ulipaji wa kodi na tozo stahiki kwa hiari.

Nawatakia Watanzania wote Kazi Njema na Heri ya Mwaka Mpya 2020
Asanteni Sana kwa Kunisikiliza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527