ALIYEKUWA RAIS WA TFF JAMAL MALINZI AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA MIWILI AU KULIPA FAINI


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na aliyekuwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh 500,000 kila mmoja ambapo wamekubali kulipa faini.


Pia mahakama hiyo imemuachia huru Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani wa TFF, Flora Rauya kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Hukumu ya Malinzi na wenzake ambao wamekaa mahabusu  kwa miaka 2 na Nusu imechukua takribani saa 5 ambapo ilianza kusomwa saa 8:30 mchana hadi saa 12 jioni.

Awali mahakama hiyo ilikwama kusoma hukumu hiyo kwa mara tatu mfululizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Hakimu aliyetakiwa kusoma hukumu hiyo kutokuwepo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, Maira Kasonde amesema amepitia ushahidi wa pande zote mbili baina ya utetezi na mashitaka ambapo amewatia hatiani washitakiwa katika makosa mawili kati ya 20.

“Kwa maana hiyo Mahakama inaona mshitakiwa wa kwanza na wa pili wana hatia kwa shitaka la tatu na mshitakiwa wa pili ana hatia katika shitaka la nne,”amesema.

Akitoa adhabu Hakimu Kasonde amesema;

“Shitaka la 3 ambalo ni kughushi nyaraka kila mshitakiwa anatakiwa kulipa faini ya laki 5 ama kifungo cha miaka miwili jela na kwa mshitakiwa wa pili katika kosa la nne la kuwasilisha nyaraka za uongo Benki anatakiwa kulipa faini ya Shilingi Laki Tano ama Jela miaka 2,” amesema.

Pia Hakimu Kasonde amesema mahakama hiyo imewakuta washitakiwa hao hawana hatia katika mashitaka 18 ikiwemo la utakatishaji fedha.

Awali kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Naye Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko amedai kuwa washitakiwa hao ni makosa yao ya kwanza kutenda na hawajawahi kushitakiwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post