WAZIRI WA KILIMO AIVUNJA BODI YA KAMPUNI YA MBOLEA TFC, ATENGUA UTEUZI WA MENEJA MKUU TFC, MKURUGENZI BODI YA KAHAWA, BODI YA TUMBAKU NA MRAJIS WA USHIRIKA


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameivunja Bodi ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) iliyoteuliwa rasmi tarehe 1 Disemba 2017 ikiwa na wajumbe sita ambao ni Mhandisi Eli Pallangyo, Bw Nuru Ndile, Bi Rosemary Msabaha, Bw Peter Shao, Dkt Kadida Mashaushi na aliyekuwa Mwenyekiti Marehemu Prof Egid Mubofu.


Waziri Hasunga amefanya maamuzi hayo leo tarehe 8 Novemba 2019 wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za Kampuni hiyo ya TFC zilizopo Masaki Jijini Dar es salaam huku akimuhamishia Wizarani Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Ndg salum Mkumba ili kumalizia mkataba wa mwezi mmoja uliosalia.


Amesema kuwa Meneja huyo anatakiwa kuripoti Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma kuanzia kesho tarehe 9 Novemba 2019 huku akieleza kuwa nafasi yake itasalia bila uteuzi mpaka atakapotoa maelekezo mengine.


Akizungumza katika kikao hicho Waziri Hasunga amesema kuwa ameivunja Bodi hiyo kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi hivyo kusababisha kampuni kushindwa kufanya biashara, kampuni kujiendesha kwa hasara hivyo kushindwa kufikia matakwa ya kuanzishwa kwa kampuni hiyo ya kuwa msambazaji kiongozi na anayeaminika kwa mbolea ya pembejeo zingine nchini kwa kuzingatia mahitaji ya mazao na afya ya udongo.


Kadhalika amesema kuwa Bodi hiyo pamoja na Meneja Mkuu imeshindwa kutekeleza wajibu wake ili kutoa suluhisho sahihi lenye gharama nafuu ya mbolea kwa wakulima na kwa wakati kwa kuzingatia hali ya udongo kwa mujibu wa Dira na Dhima ya Kampuni hiyo. Mengine ni kushindwa kuifufua na kuiendeleza kampuni hiyo


Kwa upande wa watumishi wengine wote waliobaki Waziri wa Kilimo amewapa wiki mbili kuhakikisha kuwa mbolea zilizopo bandarini zaidi ya makontena 127 ziwe zimetoka na kuwafikia wakulima kote nchini. “Tunahitaji mbolea lakini hiyo mbolea imekaa bandarini hivyo haraka iwezekanavyo ziende kwa wakulima” Alisisitiza Mhe Hasunga


Pia ametoa wiki moja kwa wafanyakazi hao kumpatia mabadiliko ya mtaji wa kampuni ili uendane na viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria za makampuni hapa nchini, kuainisha mpangokazi unaoonyesha namna watakavyopata mbolea na kuisambaza mwaka huu, namna ya kusambaza viuatilifu na jinsi ya kuvipata vingine, kadhalika namna watakavyoisaidia serikali katika usambazaji wa mbegu na pembejeo nyingine.


“Ndani ya muda huo mkiniabia mmeshindwa nitajua hamuwezi kufanya kazi hivyo nitawapa kazi watu wengine ambao wengi wapo mtaani hawana kazi na wanaweza kufanya kazi hizo” Alisema


Waziri Hasunga amesema kuwa alimpatia maelekezo Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ya mbolea (TFC) ya kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga mtambo wa kuchanganyia mbolea lakini mpaka sasa Taasisi hiyo imeshindwa kutafuta eneo hilo kwa kipindi cha karibu miezi 9.


Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amesema kuwa ataagiza wakaguzi maalumu kuikagua kampuni hiyo hususani kwenye majukumu ya kiutendaji kuangalia chanzo cha kushindwa kutekeleza majukumu yake na hatua zitachukuliwa kwa matokeo yatakayobainika.


Kadhalika amesema kuwa ametengua uteuzi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Ndg Tito Haule, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Ndg Primus Kimaryo, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Dkt Julius Ningu wote kwa pamoja ni kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao.


Waziri Hasunga amewataka watendaji hao kubadilika katika utendaji kazi ili kuongeza ufanisi na tija katika sekta ya kilimo ili kuwa na usalama wa chakula na kutofanya kazi kwa mazoea.
MWISHO



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527