ACT WAZALENDO NAO WATANGAZA 'KULEFT' KUJIONDOA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA.....



Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, ametangaza kuwa chama hicho hakitoweza kushiriki tena Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa kile alichokieleza kuwa wagombea wao zaidi la Laki 160, wameenguliwa na kubaki na wagombea Elfu 6 pekee, sawa na asilimia 4 ya wagombea wote.

Tamko hilo amelitoa leo Novemba 8, 2019, baada ya Kamati ya Uongozi wa Chama hicho kuagiza ile asilimia 4 ya wagombea wote waliopitishwa, wajiengue kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuwa haki haijaweza kutendeka.

"Sisi hatutashiriki kwa sababu tumeondolewa, toka juzi tumekuwa na mashauriano na vyama vya siasa nchini, wenzetu wametoa maamuzi yao jana, sisi tumetoa maamuzi yetu leo, tutawajulisha wananchi hatua gani tutaenda kuchukua kwa ajili ya kulinda kilicho chetu, wao wametuondoa asilimia 96 na sisi tumewasaidia kuiondoa ile asilimia 4 ili tusishiriki kabisa" amesema Zitto.

Amesema, hawatakubali Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiendelee kufurahia uchaguzi huo na kwamba chama chao kimeondolewa wagombea wake na ambapo wameachiwa asilimia nne tu (4%).

Amesema, zaidi ya wanachama 173,000 wa ACT-Wazalendo walijitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha, lakini kwenye watu wao wote, jumla ya wagombea wetu 166,000 wameondolewa.

Jana Novemba 7, 2019, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilitangaza rasmi kutoshiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, siku ya Novemba 24, ambapo pia kiliwataka wagombea wake walioenguliwa kutokata rufaa. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527