WABUNGE WANNE CHADEMA WARUDISHWA MAHABUSU....HATIMA YAO KUJULIKANA KESHO


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga kesho Jumatano Novemba 20, 2019 kutoa uamuzi dhidi ya wabunge wanne wa Chadema waliokiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani bila taarifa yoyote.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 19, 2019 na hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya washtakiwa hao kumaliza kujitetea kwa nini  wasifutiwe dhamana baada ya kukiuka masharti.

Ijumaa iliyopita Novemba 15, 2019 mahakama hiyo iliamuru wabunge hao, Mchungaji Peter Msigwa; John Heche ; Halima Mdee  na Ester Bulaya  kukamatwa baada ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili.

Wabunge hao wamerudishwa mahabusu na kutakiwa kufikishwa mahakamani hapo kesho saa 4:30 asubuhi ili mahakama hiyo itoe uamuzi.

Amri ya kukamatwa ilitolewa na Hakimu Simba baada ya washtakiwa hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote wala wadhamini wao.


Wakijieleza kwanini wasifutiwe dhamana kwa nyakati tofauti akianza Msigwa aliomba radhi kwamba haikuwa nia yake kuidharau mahakama, tangu kesi ianze hajawahi kuchelewa, hajawahi kukaidi amri ya mahakama na kwamba anaheshimu kiti cha hakimu.

Amedai alitokea Dodoma alidhani kesi ni saa nne na nusu kama kawaida akiwa na Heche lakini walipofika walikuta kesi imeisha na jitihada za kumuona hakimu kumaliza tatizo hilo zilishindikana.

Kwa upande wake Mdee pia ameomba radhi, ameonyesha jinsi anavyoiheshimu mahakama na kwamba alichelewa kwa kuwa alipitia kupima presha zahanati na alipofika kesi ikawa imeisha na amri imeshatolewa na wadhamini wake waliwahi lakini hawakufanikiwa kumaliza tatizo hilo Novemba 15 kwa kuwa waliambiwa amri ilishatolewa.

Heche amedai aliomba asifutiwe dhamana, anadai anaheshimu mahakama, hajawahi kuidharau, siku ya kesi ilikuwa Dar es Salaam lakini alijua kama kawaida kesi yao inasikilizwa saa nne na nusu hivyo alipofika alikuta imeahirishwa.

Akijitetea Bulaya amedai Novemba 14 alienda msibani Singida kumzika mama yake mdogo lakini aliwapa taarifa wadhamini wake ambao siku ya kesi walikuwepo katika eneo la mahakama.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527