BAADA YA CHADEMA KUJIONDOA... VYAMA VINGINE 11 VYA SIASA TANZANIA VYATANGAZA KUSHIRIKI UCHAGUZI.. 'ANAYESUSA KULA AMESHIBA'

 Vyama 11 vya upinzani visivyo na uwakilishi katika Bunge la Tanzania vimetangaza kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 vikieleza kuwa, “anayesusa chakula ameshiba.”

Vimetangaza uamuzi huo leo Ijumaa Novemba 8, 2019 jijini Dar es Salaam siku moja baada ya Chadema kujitoa kushiriki uchaguzi huo kutokana na figisufigisu zilizofanyika katika uchukuaji, urejeshaji wa fomu za kugombea na uteuzi wa wagombea.

Vyama hivyo ni DP, NRA, AFP, Demokrasia Makini, UDP, ADC, Ada- Tadea, Sauti ya Umma (Sau), TLP, CCK na UMB

Vimesema vitashiriki vikiamini Wizara ya Tamisemi inayosimamia uchaguzi huo itatenda haki kwa kuwarejesha wagombea wake walioenguliwa kushiriki uchaguzi huo.

“Tunaamini watarudishwa kwa sababu wamekidhi matakwa. Tunataka tushindane kwa hoja na sera kwenye mikutano ya hadhara,” amesema katibu mkuu wa DP, Abdul Mluya kwa niaba ya viongozi wa vyama hivyo.

Amesema, “tutaendelea na uchaguzi kwa sababu siku zote anayesusa chakula ameshiba. Hatuwezi kususia uchaguzi kwa sababu ni mtaji wa kujiimarisha hasa kwa vyama hivi ambavyo havina diwani wala wabunge tofauti na Chadema.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527