TIGO YATANGAZA KUUNGANA RASMI NA ZANTEL


Hatua hiyo itasaidia kuboresha zaidi huduma na kukuza sekta ya mawasiliano nchini.

Dar es Salaam. Novemba 4, 2019. Kampuni ya Mawasiliano ya MIC Tanzania Public Limited Company (Tigo), leo imetangaza rasmi kuungana na kampuni ya Zanzibar Telecom Public Limited Company (Zantel) baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na kiumiliki ambapo lengo kuu ni kukuza na kuboresha huduma za mawasiliano nchini.

Pamoja na kupata vibali kutoka mamlaka zinazohusika, mchakato wa kuhamisha hisa na umiliki kamili kutoka Zantel kwenda Tigo sasa umekwisha kamilika. Kufuatia kukamilika kwa zoezi hili sasa makampuni haya yataunganisha shughuli zake za kiutendaji Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Akizungumza kuhusu muungano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Simon Karikari alisema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa; “Ninaamini kuwa kuunganishwa kwa kampuni hizi - Tigo na Zantel kutajenga huduma jumuishi kwa watanzania wote siku za usoni. Wateja wote wa Tigo na Zantel wataweza kufurahia huduma bora kutoka kwenye soko imara litakalosaidia kuchochea ubunifu kwenye sekta ya mawasiliano,” alisema Karikari. 

Muunganiko wa makampuni haya mawili utasaidia katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wa Tigo na Zantel waliopo kote Tanzania Bara na Visiwani. Aidha, muungano huu utawezesha kupanua wigo wa huduma zetu pamoja na kuongeza ubora wa upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya mijini na vijijini. Vile vile muungano huu utasaidia katika usambazaji wa huduma za mawasiliano kwa makampuni na taasisi mbalimbali nchini na pia kupanua huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi. 

Tunategemea mafanikio chanya kutokana na muunganiko wa makampuni haya mawili wenye lengo la kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa. 

Zoezi la kuunganisha taratibu za kiutendaji wa makampuni haya mawili zinatazamiwa kuanza hivi punde. Aidha, wateja wa Tigo na Zantel wataendelea kupata huduma bila usumbufu wowote kutoka mtandao husika kwani namba na laini za wateja hazitabadilika.

Tigo
Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo ni kampuni inayoongoza katika utoaji wa huduma kidigitali hapa nchini.Tigo ilianza kutoa huduma zake mwaka 1995 ikiwa na huduma mbalimbali za sauti, jumbe (SMS), intaneti yenye spidi pamoja na huduma za kifedha.

Tigo imekuwa mstari wa mbele kuleta mapinduzi ya kidigitali ikiwamo kuanzisha Smartphone ya Kiswahili, Facebook ya bure, App ya Tigo Pesa na zaidi kuwa kampuni ya Kwanza kutoa huduma ya kutuma na kupokea pesa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527