TAARIFA KWA UMMA TOKA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS)


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unatoa wito kwa umma kuchukua tahadhari na matumizi ya moto kwenye maeneo yanayokaribiana na misitu. Tunawaomba wananchi wote wakiwemo wavunaji, warina asali, wawindaji, wafugaji na hususani wakulima kuepuka matumizi ya moto katika kuandaa mashamba kwani wamekuwa ni chanzo kikuu cha moto unaoingia kwenye misitu hasa kunapokuwa na upepo mkali.


Tunapenda kuuarifu umma kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la matukio ya moto katika mikoa ya Iringa na Njombe iliyopelekea kuunguza mashamba ya miti ya watu binafsi na yale ya serikali hususani shamba la miti la Sao Hill lililopo katika wilaya ya Mufindi. Moto huo umeunguza sehemu tofauti za msitu huo na kusababisha hasara kufuatia kuungua miti ya umri tofauti.

TFS inapenda kutoa pole kwa wadau waliounguliwa vifaa vyao vya uvunaji pamoja na mazao yaliyovunwa wakati mashine ya kuangushia miti (chainsaw) ilipolipuka ghafla katika moja ya tukio lililopelekea kusambaa kwa moto. 

Aidha, tunatoa shukrani nyingi sana kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama (W) Mufindi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), JKT Mafinga, Jeshi la zimamoto, Jeshi la Akiba, wavunaji wa shamba la Sao Hill, vikosi vya moto vya shamba, watumishi wa TFS na wananchi wote wa maeneo jirani kwa ushirikiano wao wa hali na mali katika kupambana na moto. 

Katika hatua hiyo ninawakumbusha tena kwa mara nyingine waandaaji wa mashamba kuhakikisha kuwa wanapata vibali vya matumizi ya moto kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 kama sehemu ya kukabiliana na changamoto hii.

Tunatoa wito kwa wananchi wote kuepuka shughuli zozote ambazo zinaweza kupelekea au kusababisha moto kwenye misitu ya asili au ya kupanda kwani moto ni adui namba moja wa misitu yetu.


Imetolewa na
Prof Dos Santos Silayo
KAMISHNA MHIFADHI - TFS


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527