RAIS MAGUFULI AMPA MAAGIZO MAZITO CAG MPYA....." USIJIFANYE MUHIMILI...SIKUTISHI....."


Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere, leo Novemba 4 ,2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumpa maagizo katika kazi yake mpya.

Moja ya maagizo aliyompa ni kuhakikisha anasuka upya uongozi ndani ya taasisi hiyo ili kuhakikisha kuwa inafanya kazi kulingana na sheria na maagizo ya mihimili inayoongoza nchi. 

Maagizo mengine aliyopewa ni, "CAG nenda kafanye kazi huko, usije ukajifanya na wewe ni muhimili mwingine, mihimili ni mitatu na umeshaiona hapa. Nafasi yako ni Mkaguzi Mkuu wa Serikali, kafanye kazi zako vizuri bila ya kuonea watu. 


“Unapopewa kazi na mihimili mingine kama Bunge au Mahakama kaitekeleze usibishane nao wewe ni mtumishi. Kasimamie hiyo ofisi kuna baadhi ya watendaji wako wanapokwenda kukagua kwenye balozi wanaomba fedha, sasa nenda kawachambue.” Amesema Rais Magufuli.

Aidha, amesema Rais ana mamlaka ya kumtoa CAG kulingana na Katiba na Sheria akieleza kuwa upo uwezekano wa mtumishi wa nafasi hiyo kutolewa muda wowote hata chini ya miaka mitano.

“Nenda ukachape kazi, katika maisha ya duniani huwezi kupewa mamlaka ya kuteua halafu usiwe na mamlaka ya kutengua, ukishindwa hivyo huwezi kuwa Rais. Mwenzako aliyekuwepo amemaliza muda wake leo, kwa hiyo kesho uende ofisini ukaanze kazi, kayatoe mauchafu yote utakayoyakuta mengine waulize Wizara ya Fedha wanayafahamu,” amesema Rais.

"Unaweza kumaliza miaka yako mitano au ukaishia mmoja. katika maisha ya duniani huwezi ukapewa mamlaka ya kuteua halafu usiwe na mamlaka ya kutengua, sikutishi lakini wewe nenda kafanye kazi zako" 

Kuhusu suala la rushwa, Rais Magufuli amesema, "lakini pia kasimamie hiyo ofisi kuna baadhi ya watendaji wako wanapotumwa kwenda kukagua kwenye balozi wanalipwa pesa hapa na wakifika huko nako wanaomba pesa. Ofisi ya CAG sio clean (safi) kama mnavyofikiria, sasa nenda kachambue ukapange positions (nafasi) za watu wako, ili mauchafu (uchafu) haya ukayasafishe.

“Una heshima umetolewa kwenye Ukamishna wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) hukusema neno ukaenda kufanya kazi huko, wapo wengine ukiwateua utadhani nafasi zao unampa UDC (Ukuu wa Wilaya) ukimtoa anaanza kulalamika,” amesema Rais Magufuli.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527