SERIKALI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO SEKTA YA USAFIRISHAJI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Asasi za Kiraia ziendelee kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi.

“Nitoe rai kwenu wana AZAKI, muendelee kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla ili Serikali iweze kujenga miradi mikubwa ya kijamii,” amesema.

Ametoa wito huo leo jioni (Jumatatu, Novemba 4, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na washiriki wa Maonesho ya Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini yaliyoanza leo kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Maonesho hayo yatafikia kilele chake Ijumaa, Novemba 8, mwaka huu.

Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya Kiserikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini kama vile kuwajengea uwezo viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo Madiwani, viongozi wa vijiji na mitaa ili watambue majukumu yao.

“Niwatoe hofu tu kwamba Serikali inatambua mchango wenu wa kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo; kujiongezea kipato na kupata ujuzi; utoaji wa huduma za kijamii hususan elimu, afya, upatikanaji wa maji, huduma za kisheria na huduma za mikopo midogo.

“Pia tunatambua mchango wa AZAKI wa kuleta teknolojia mpya na rahisi kwa wananchi pale mnapoona kuna uhitaji. Pia mnaisaidia Serikali kupinga mila potofu na kandamizi hasa kwa makundi yenye mahitaji maalum,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzitaka AZAKI nchini zizingatie sheria iliyofanyiwa marekebisho ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24/2002 na kanuni zake, ambayo ilipitishwa na Bunge kupitia Sheria Na. 3/2019 na kusisitiza kwamba marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta hiyo.

“Nipende kuwahakikishia wana-AZAKI kuwa marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta ya NGOs na siyo kuyabana mashirika yasiyo ya Kiserikali kama ambavyo imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya watu. Marekebisho hayo yalizingatia misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” amesema.

Kuhusu mapato ya AZAKI, Waziri Mkuu amesema fedha wanazopata zinaweza kufanya miradi mikubwa ambayo itawanufaisha wananchi na akawasihi wazitumie kwenye ujenzi wa miradi mikubwa inayoonekana badala ya kuendesha semina na warsha.

“Tunajua fedha mnazopata zinaweza kusaidia kwenye miradi hii. Kwa mfano, kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu, tulifanya mapitio ya ufadhili wa fedha mnazopata. Na katika upekuzi uliofanyika kwenye taasisi 92, ilibainika kwamba zilipokea jumla ya sh. bilioni 261.059 ambazo zimeingia kwenye AZAKI hizi.”

“Vilevile, mwaka 2016 hadi 2017, tuliangalia mapato ya NGOs 51, tukagundua kuwa katika kipindi cha miaka miwili, zimepokea jumla ya shilingi trilioni 2.5. Kama fedha hizi zote zingeratibiwa vizuri kwa kupunguza matumizi yasiyo na umuhimu ni lazima tungefika mbali. Tutumie vizuri fedha hizi za ufadhili kwa miradi inayoonekana,” amesisitiza.

Akizungumzia kuhusu ajira kwa vijana, Waziri Mkuu amesema vijana ni kundi lenye umuhimu mkubwa katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo licha ya kuwa wanakabiliwa na uhaba wa ajira.

Amesema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha asilimia 35 ya Watanzania wote ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35. Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa nguvukazi ya Taifa wa mwaka 2014, vijana wamebainika kuwa ndio kundi kubwa la nguvukazi ya Taifa ambao ni asilimia 56 ya nguvukazi yote nchini.

“Kila mwaka, kumekuwa na ongezeko la vijana wanaoingia kwenye soko la ajira. Kwa mfano, taarifa ya hali ya ajira ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa mwaka 2019 inaonesha kuwa asilimia 11.8 ya nguvukazi ya vijana duniani ambao ni takriban vijana million 59.1 hawana kazi,” amesema.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Suleiman Jafo alizishukuru asasi zote za kiraia ambazo zinafanya kazi Tanzania kwa sababu zinawahudumia wananchi kwa karibu zaidi. “Ninazishukuru NGOs zote kwa kusaidia kutoa elimu kwa wananchi. GTunazishukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya Tanzania nzima kwa kushirikiana na Ofsi ya Rais TAMISEMI,”

Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema mwaka huu, wizara yake imesajili mashirika yasiyo ya Kiserikali 617 ikilinganishwa na mashirika 385 yaliyosajiliwa mwaka 2017.

“Kati ya hayo mashirika 617, mashirika 44 ni ya ngazi ya kimataifa; 551 ni ngazi ya kitaifa, saba ni katika ngazi ya mikoa na mashirika 15 ni katika ngazi ya wilaya. Hadi kufikia Oktoba, 30, 2019, tumeshasajili mashirika 19,318” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527