RAIS MAGUFULI ATUNUKIWA SHAHADA YA UDAKTARI WA FALSAFA UDOM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amesema alitumia muda mrefu kufikiria kukubali ombi la kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa kutokana na Jitihada, anazofanya katika kuiletea maendeleo Tanzania pamoja na mapambano dhidi ya Rushwa, ambapo amesema alitumia mwezi mmoja kukubali ombi hilo.


Rais Magufuli amesema kuwa sababu kubwa iliyomfanya kukaa kwa muda mrefu ni kile alichokisema, ni imani yake ilikuwa ikimsuta juu ya kutopenda vitu vya bure, kama alivyokuwa amefundishwa na Baba yake mzazi pindi alipokuwa mdogo.

Akiongea baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa ameyasema haya; “Baada ya kuambiwa kwamba nitatunukiwa shahada ya Udaktari wa Falsafa nilijiuliza maswali mengi, lakini baada ya kukumbuka kuwa mara nyingi shahada hizi za heshima hazitolewi kwa maana ya kumpa mtu binafsi bali zinakuwa kwa niaba ya watu wengine”

“Sijawahi sana kupewa vitu vya burebure ama vitu vya dezo kwa Kiswahili cha mjini, nakumbuka zamani hata nikienda kuomba hela ya kalamu baba alikuwa hanipi kirahisi, alinipa kazi ya kufanya kama vile kuchunga ng’ombe ili akikupa hela na wewe uwe umeilipia”

“Lakini baadaye nikasema nikubali kutunukiwa kwa heshima ya Rais Mstaafu Mkapa (Mkuu wa UDOM) na sababu ya pili niliona kuwa shahada hii ya heshima niliyopewa ni heshima si tu kwangu bali kwa wote waliowezesha mafanikio tuliyofikia kwa miaka hii minne”

“Shahada hii kimsingi imetolewa kutokana na mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano, mafanikio hayo hayatokani na juhudi zangu binafsi bali kwa ushirikiano wa Watanzania wote”

“Tunaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa takribani kilomita 700 kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora kwa gharama ya Tsh. tril. 7.062, upanuzi wa viwanja vya ndege 11, pia upanuzi wa bandari zetu kubwa tatu za Dar, Mtwara na Tanga kwa gharama ya Tsh tril. 1.2”

“Miradi ya REA, wakati tunaingia madarakani ni vijiji 2,118 ndivyo vilikuwa na umeme, sasa ni vijiji zaidi ya 8,000 vimeshapelekewa umeme”

“Kutokana na juhudi zetu, tumeendelea kupata mafanikio, uchumi wa nchi yetu unaendelea kuimarika ambapo kwa sasa unakua kwa wastani wa 7% na kuifanya nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika”

“Kutokana na kuimarika kwa miundombinu na huduma za usafiri, idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii milioni 1.2 hadi kufikia zaidi ya milioni 1.5 mwaka jana”

“Nafurahi kuona mwitikio wa viwanda ni mkubwa, hadi sasa viwanda 4,000 vimejengwa kote nchini, pamoja na ukuaji wa sekta nyingine katika kuchangia uchumi wa taifa letu, ukuaji wa sekta ya viwanda ni muhimu na unawezesha mambo mbalimbali”

“Katika kipindi cha miaka minne nchi yetu imeweza kuvutia mitaji ya uwekezaji yenye thamani ya takribani Dola za Kimarekani Bilioni 13 sawa na Tsh. Tril. 30 na kutoa ajira nyingi, na asilimia kubwa ya uwekezaji umeelekezwa katika sekta ya viwanda”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527