POLISI SHINYANGA WAKAMATA POMBE KALI IKIWA IMETELEKEZWA PORINI KUKWEPA KODI...RC TELACK AWA MBOGO



Na Marco Maduhu - Malunde 1 blog
Serikali mkoani Shinyanga imekamata pombe kali aina ya Shujaa, ambayo ilikuwa imetelekezwa porini eneo la Lubaga manispaa ya Shinyanga, ikiwa ndani ya gari aina ya Roli lenye namba za usajili T 391 AES, kwa madai ya kukwepa kulipa kodi.


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Novemba 9, 2019 Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwa kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Shinyanga, eneo ambalo gari hilo limewekwa chini ya ulinzi, amesema kuwa serikali itawashughulikia wawekezaji wote ambao wanatabia ya kukwepa kulipa kodi ya serikali.

Telack ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga, amesema Serikali inahitaji sana wawekezaji hapa nchini ili kukuza uchumi wa taifa, lakini siyo wawekezaji wa kukwepa kodi na kufanya biashara kiujanja ujanja.

“Pombe hii kali ya Shujaa Katoni 1,490 tumeikamata ikiwa imefichwa porini eneo la Lubaga manispaa ya Shinyanga, ikiwa ndani ya gari hili ambalo mnaliona hapa, na wamiliki wa kiwanda hiki wamekuwa na tabia ya kukwepa kulipa kodi na siyo mara ya kwanza kukamatwa,”amesema Telack.

“Hivyo naagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Kesho wafike hapa, ili kufanya tathmini ya kujua kiasi gani cha kodi ambacho watu hawa wanapaswa kulipa, ili Serikali iweze kukusanya mapato na kupata fedha za kutekeleza maendeleo kwa wananchi,”ameongeza.

Pia ameonya baadhi ya Askari Polisi kushirikiana na waharifu hao wa kiwanda cha Shujaa, na kuwapa mbinu za kukimbia ili kukwepa mkono wa Serikali, na kumuagiza Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Shinyanga, kuwa ndani ya siku nne, wamiliki wa kiwanda hicho wawe wameshakamatwa.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Richard Abwao, alithibitisha kukamata Pombe hiyo ya Shujaa, na kuahidi kutekeleza maagizo hayo ya mkuu wa mkoa, huku akitoa wito kwa wamiliki hao wa kiwanda cha Shujaa wajisalimishe wenyewe kwa usalama wao kwani watakamatwa tu popote pale walipo.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI


Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akionya wawekezaji kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi za Serikali hasa kiwanda hicho cha Pombe Kali ya Shujaa, kushoto ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, na nyuma yake ni gari likiwa na Pombe za Shujaa.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akisisitiza zoezi hilo la kusaka bidhaa ambazo hazilipi kodi ni endelevu ambapo wamiliki wa kiwanda hicho cha Pombe ya Shujaa siyo mara ya kwanza kukamatwa na umekuwa mtindo wao wa kukwepa kulipa Kodi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Richard Abwao, akithibitisha kuikamata Pombe hiyo ya Shujaa ikiwa porini na kuahidi kuwatia nguvuni wahusika ambao wamekimbia.

Pombe kali za Shujaa Katoni 1,490 zikiwa kwenye Gari eneo la kituo cha Polisi wilaya ya Shinyanga.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack mkono wa kulia, akiwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko Kushoto wakiangalia Pombe hiyo Kali ya Shujaa.


Picha na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527